Akemea vurugu Uchaguzi Mkuu

01Aug 2020
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Akemea vurugu Uchaguzi Mkuu

SHEIKH Balilusa Khamis wa mjini Shinyanga, amewataka viongozi wa vyama vya kisiasa nchini na wanachama wao, kutanguliza mbele maslahi ya taifa na kutofanya vurugu wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Alitoa rai hiyo jana baada ya kuongoza ibada ya sikukuu ya Eid Al Hajj iliyofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru mjini hapa, akibainisha kuwa, matarajio ya viongozi wa dini ni kuona uchaguzi huo unakuwa huru na utulivu unakuwapo.

Sheikh Khamis ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Shinyanga, alisema viongozi wa siasa na wanachama wao, wanapaswa kutanguliza maslahi ya taifa mbele na siyo maslahi yao binafsi katika kipindi chote cha uchaguzi huo.

“Sisi kama viongozi wa dini, tunawaomba sana viongozi wa kisiasa hapa nchini pamoja na wanachama wao, katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, watangulize maslahi ya taifa na siyo maslahi yao binafsi, ili kulinda amani ya nchi yetu na kutofanya vurugu zozote kwenye uchaguzi,” alisema.

Shekh Khamis pia aliwataka wakuu wote wa shule binafsi kutowanyima wanafunzi muda wa kwenda kusali, kwa madai ya kufidia muda uliopotea wakati wa likizo ya lazima kupisha corona.

Mjumbe wa Baraza la Masheikh mjini Shinyanga, Sheikh Khalfan Ally, akitoa mawaidha, aliwataka waumini wa dini ya Kiislam hasa vijana, kuzingatia miiko na sheria ya dini hiyo, ili kutoporomoka kimaadili na kuacha kuzaa watoto kabla ya kufunga ndoa.

Alisema baadhi ya vijana wa dini hiyo hawana maadili kabisa, ambapo wamekuwa wakifanya uzinzi na kuzaa watoto nje ya ndoa, kutovaa mavazi ya heshima, kunyoa mitindo ya ovyo ya nywele na kupenda maisha rahisi kwa kuoa wanawake wenye pesa.

Habari Kubwa