Akinamama wampongeza Rais Samia kuwaboreshea huduma za afya

13Oct 2021
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Akinamama wampongeza Rais Samia kuwaboreshea huduma za afya

AKINAMAMA wa Salawe wilayani Shinyanga, wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassani, kwa kutoa fedha kwa ajili ya kuwaboreshea huduma za afya katika kituo cha Afya Salawe wilayani humo, ili waondokane na kufuata huduma umbali mrefu hasa kwa akina mama wajawazito.

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akiongoza wananchi wa Salawe wilayani humo, kuchimba Msingi kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na Maabara, kwa ajili ya kuboresha huduma za afya.

 

Mmoja wa akina mama hao Modesta Charles, ambaye pia ni mhudumu wa afya ngazi ya jamii, amebainisha hayo leo wakati Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, alipokuwa akishirikiana na wananchi kuchimba msingi kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wanje (OPD), na maabara katika kituo cha Afya Salawe.

Wamesema kituo hicho cha afya ni kidogo na hakina majengo ya kutosha, wala kuwapo na huduma ya upasuaji, ambapo akina mama wajawazito wanapofika kujifungua hupata shida, hasa wale ambao wanakutwa na tatizo la kufanyiwa upasuaji, na kulazimika kwenda Hospitali ya wilaya umbali mrefu na kuhatarisha maisha yao.

“Tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassani kwa kutoa fedha za uboreshaji wa kituo hiki cha afya Salawe, ambapo akina mama Wajawazito wataondokana na adha ya kufuata huduma bora za afya umbali mrefu zaidi ya kilomita 70,”amesema Charles.

Akina mama wa Salawe wilayani Shinyanga, wakishirikiana na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, kuchimba Msingi kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la wagonjwa wa nje na maabara, ili kuwaboreshea huduma za afya.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko, amewapongeza wananchi kuchangia nguvu kazi ya kuchimba msingi wa majengo hayo mawili, OPD na Maabara, na kusema hiyo ni hatua ya awali, ambapo Serikali itaendelea kuboresha huduma za afya zaidi ikiwamo upatikanaji wa madawa na madaktari.

Aidha, amesema ujenzi huo wa jengo la wagonjwa wanje, Maabara, na kichomea taka, fedha zake zimetolewa na Rais Samia Suluhu Hassani Sh. milioni 250, na kuwataka mafundi wajenga kwa kiwango bora kulingana na thamani ya fedha, pamoja na kumaliza kwa wakati.

Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Dk. Mameritha Basike, amesema uboreshaji wa huduma za afya wilayani humo, utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza pia vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na uzazi, na kujata Takwimu kuwa Mwaka jana akina mama 14 walipoteza maisha, na mwaka huu wapo wawili.

Habari Kubwa