Alidai wahudumu wa ATCL hawana mvuto, aomba radhi watanzania

14Nov 2019
Gwamaka Alipipi
Dodoma
Nipashe
Alidai wahudumu wa ATCL hawana mvuto, aomba radhi watanzania

MBUNGE wa Uvinza ( CCM), Hasna Mwilima, amewaomba radhi Watanzania wote hususani wanawake kwa kauli yake aliyowahi kutoa bungeni kuwa wahudumu wa Shirikia la Ndege la Tanzania hawana mvuto.

Mbunge wa Uvinza, Hasna Mwilima

Mwalimu amesema aliitoa kauli ile kwa nia nzuri ya kuliboresha Shirika la Ndege na siyo kuwadhalilisha wanawake.

Ametoa kauli hiyo leo bungeni mjini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali na majibu, kabla hajaanza kuuliza swali, hali iliyosababisha idadi kubwa ya wabunge kumshangilia.

"Naomba nichukue nafasi hii kuwaomba radhi Watanzania wote hususani wanawake wenzangu kwa kauli yangu niliyowahi kuitoa ya kuwadhalilisha," amesema Mwilima.

Kutokana na kauli ya Mwilima ilimlazimu Spika wa Bunge, Job Ndugai kusema: “Huu ndiyo uungwana waheshimiwa wabunge, Mheshimiwa Mwilima Bunge limekusamehe sasa endelea kuuliza swali lako".

Mwilima amezua tafrani ndani ya Bunge baada ya kulitaka shirika hilo kuajiri wahudumu wenye mvuto.

Wakati akichagia, Mwilima amesema wahuduma wa shirika hilo hawana mvuto, wafupi, hali ambayo husababisha ndege kutokuwa na mvuto zaidi.

“Wahudumu wetu kwenye Shirika letu la ndege utakuta Air hostess mfupi, hana mvuto, mhudumu nyuma yupo kawaida, hata mimi na miaka yangu ni 50 nimeshazeeka nilivyo ninavutia, Tunapoajiri ma-Air hostess akiwa ndani ya ndege ukimuita akigeuka abiria anaona kweli,” amesema Mwilima.

Hoja hiyo, ilimlazimu Naibu Waziri wa Ujenzi, anayeshughulikia sekta ya Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa Serikali haitumii kigezo cha mvuto katika kuajiri watumishi wa ATCL.

Habari Kubwa