Alimwa faini Mil. 5/- kisa ujumbe kwenye Facebook

16Nov 2017
Hellen Mwango
Nipashe
Alimwa faini Mil. 5/- kisa ujumbe kwenye Facebook

BOB Chacha Wangwe amenusurika kwenda jela kutumikia kifungo cha mwaka mmoja na nusu baada ya kulipa faini ya Sh. milioni tano kwa kukutwa na hatia ya kosa la kutuma ujumbe wenye taarifa ya uongo kupitia kurasa za mtandao wa Facebook.

Hukumu hiyo ilitolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana, baada ya ushahidi wa Jamhuri kuthibitisha makosa dhidi yake.

Hukumu hiyo ilisomwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Bob ni mwanaharakati na mtoto wa marehemu Chacha Wangwe, ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Tarime, mkoani Mara na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) -Bara.

Hakimu alisema katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri uliita na mashahidi 6 na vielelezo 5 na utetezi mmoja.

Alisema  Mei 7, 2016 polisi walipata taarifa ya chapisho la Bob, wakaanza kumfuatilia na kumkamata kisha walichukua simu na kuipeleka Polisi kuikagua.

"Katika utetezi wako, Bob hukupinga kuandika maneno hayo lakini umedai kuwa hukuyachapisha katika jamii bali yalikuwa ni siri kwenye akaunti yako… simu yako ilipopekuliwa  ilionyesha imetumika kuchapisha ujumbe huo kwa jamii na watu walikujibu, ikiashiria ujumbe uliwafikia," alisema hakimu na kuongeza:

"Mahakama hii imeona ni wazi kuwa mshtakiwa   ulikuwa na nia ya kuchapisha taarifa hiyo, kueleza kile ambacho ulikiona sahihi kama ingekuwa ni ujumbe wako binafsi basi polisi wasingeweza kukutafuta, na watu wasingekujibu".
 
Hakimu Shaidi alisema kutokana na ushahidi huo, Bob amekutwa na hatia chini ya kifungu cha 16 cha sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015.

Katika utetezi wake, Bob aliomba apunguziwe adhabu kwa sababu ni mwanafunzi wa masomo ya sheria, pia ni kijana mdogo na ni kosa lake la kwanza kulitenda.

Hakimu Shaidi alisema anakubaliana na hoja za Bob, kwani mahakama inamuona bado ni mdogo na anapaswa kufanya mambo mengi mazuri katika jamii.

Pia alisema kama yeye ni mwanafunzi wa masomo ya sheria, anapaswa kufanya mambo mema katika jamii ili wengine wamuige.

"Mshtakiwa unatakiwa kuwa mfano mzuri kwa jamii ili uweze kufika mbali katika taaluma hii ya sheria," alisema.

"Hivyo mahakama inakuhukumu kulipa faini ya Sh. milioni 5 ama uende jela mwaka mmoja na nusu… pia milango ya dhamana ipo wazi," alisema hakimu Shaidi wakati akimalizia kusoma hukumu hiyo.

Katika kesi hiyo namba 167, Wangwe anatuhumiwa kosa la kuchapisha taarifa za kupotosha katika ukurasa wake wa mtandao wa Facebook.

Inadaiwa alitenda kosa hilo March 15, 2016 ambapo alichapisha taarifa iliyosema:

“….Tanzania nchi ambayo inajaza chuki wananchi.… matokeo ya kubaka Demokrasia Zanzibar ni hatari zaidi ya Muungano wenyewe…. Haiwezekani nchi ya Zanzibar kuwa koloni la Tanzania Bara kwa sababu za kijinga.”

Baada ya hukumu hiyo, Wakili wa utetezi Benedict Ishabakaki, alisema hawajaridhika na hukumu hiyo na kwamba watakata rufani.
Alisema maneno hayo hayakuwa ya uchochezi na kwamba mahakama haijamtendea haki Wangwe kwa kumtia hatiani.

Habari Kubwa