Alivyouawa akijibizana risasi na polisi

22May 2020
Hamida Kamchalla
Tanga
Nipashe
Alivyouawa akijibizana risasi na polisi

MTU mmoja anayesadikiwa kuwa jambazi ameuawa na polisi mkoani hapa huku mwingine akijeruhiwa baada ya majibizano ya risasi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Blasius Chatanda, akionyesha bunduki aina ya shortgun, kwa waandishi wa habari, ofisini kwake, jana, baada ya kuikamata mikononi mwa watuhumiwa wa ujambazi pamoja na silaha nyingine. PICHA: HAMIDA KAMCHALLA

Kamanda wa polisi mkoani hapa, Blasius Chatanda, alisema mtu huyo alikuwa akipanda juu ya ukuta tayari kwa kuvamia nyumba na kuiba akiwa na bunduki aina ya shotgun huku mwenzake akiwa chini kumuwekea ulinzi.

Alisema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana saa tisa katika mtaa wa Mbolea, kata ya Ngamiani kati, ambako majambazi hao walivamia nyumba ya Jamali Mbarouk (60), mfanyabiashara.

Alisema baada ya majambazi hao kuvamia nyumba hiyo askari polisi walikuwa doria na walipowaona waliwazingira na kuanza kupambana na majibizano ya risasi huku jambazi huyo aliyejulikana kwa jina maarufu 'Macho makavu' alipigwa risasi na kufariki papo hapo.

Alisema wakati wanajiandaa kumkabili jambazi mwingine walifanikiwa kumpiga risasi na kumjeruhi, lakini aliokolewa na wenzake waliokuwa nje ya nyumba huyo kwa njia isiyojulikana.

Kamanda alibainisha kuwa majambazi hao kabla hawajafanya tukio hilo, walishafanya mauaji ya mlinzi wa ofisi ya Brac, mtaa wa Usagara na kuvunja ofisi hiyo, na kuiba Sh. 200,000.

Vilevile Chatanda alitoa rai kwa wananchi mkoani hapa na kusema kuwa ili jeshi la polisi liweze kufanya kazi zake kwa ufanisi na kuwalinda raia na mali zao inawapasa waendelee kushirikiana kwa ukaribu na kutoa taarifa kwa jeshi hilo bila kuhofia.

Alisema yeyote atakayejihusisha na vitendo vya kihalifu hatoweza kudumu kwa kuwa jeshi hilo limejipanga kukabiliana na uhalifu ndani ya mkoani na hata kwenye mipaka yake.

Aliwataka wananchi wawe na amani katika kusherehekea sikukuu huku akiwaasa kutofanya misongamano ili kuendelea kujikinga na maambukizo ya corona.

"Tumeendelea kuimarisha ulinzi hasa pale Horohoro na tunawahakikishia wananchi wafanye kazi zao kwa amani pia katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu washerehekee kwa amani bila hofu ya kuvamiwa, lakini tusifanye misongamano kwenye kumbi za tarehe," alisisitiza.

"Disko toto marufuku, atakaeleta tamaa ya kufungua kumbi kwa ajili ya kupiga muziki na kuwakusanya watoto tutamshughulikia, tusiwaache watoto watembee peke yao hasa huko kwenye maeneo ya fukwe, mnaweza kuanza kusherehekea vizuri mwisho wake ukawa mbaya," alisema.

Habari Kubwa