Aliwa na mamba akivua samaki

16Jan 2019
Ahmed Makongo
Bunda
Nipashe
Aliwa na mamba akivua samaki

KIJANA Said Hussein (22), mkazi wa kijiji cha Kasuguti, Bunda mkoani Mara, amekamatwa na kuliwa na mamba wakati akivua samaki katika Ziwa Victoria.

Diwani wa Kasuguti, Alex Paul, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Jumamosi iliyopita katika mwalo wa kijiji hicho, majira ya saa tatu usiku, wakati kijana huyo alipokuwa anavua samaki na mwenzake mmoja.

Paul alisema wakati vijana hao wakiendelea na uvuvi, ghafla mamba alitokea na kumkamata Said na kutokomea naye kusikojulikana.

“Baada ya mamba huyo kumkamata Said, mwenzake alipiga kelele za kuomba msaada na wananchi walifika, lakini hawakufanikiwa kumwokoa kwa sababu alitokomea naye kusikojulikana,” alisema.

Alisema wananchi walifanya juhudi za kumtafuta usiku huo, lakini hawakumpata, ambapo mabaki ya mwili wake yalipatikana juzi zikiwa zimepita siku tatu tangu alipokamatwa.

“Tulimtafuta siku tatu mfululizo na tukafanikiwa kupata mwili wake eneo la mtoni ukiwa umeliwa sehemu mkubwa,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, diwani huyo alitoa wito kwa wananchi wa kata hiyo wanapofanya shughuli za uvuvi wawe makini na kuchukua tahadhari kwa kuwa mamba ni wengi katika eneo hilo.

Alisema vijana hao hawakuwa na mtumbwi bali walikuwa kwa miguu tu, jambo ambalo lilifanya mamba huyo amkamate mmoja wao kwa urahisi.

“Natumia nafasi hii kutoa rai kwa wananchi pindi wanapoendesha shughuli hizo za uvuvi wawe wanachukua tahadhari na kuwa na vyombo vya kuvulia. Kwa mfano hao vijana walikuwa wanavua kwa miguu tu bila kuwa na mtumbwi,” alisema.

Habari Kubwa