Aliyeachiwa na Rais auawa kwa ujambazi

22Jan 2020
Godfrey Mushi
Mwanga
Nipashe
Aliyeachiwa na Rais auawa kwa ujambazi

MFUNGWA aliyeachiwa huru kwa msamaha wa Rais John Magufuli kutoka Gereza Kuu la Karanga mkoani Kilimanjaro, ameuawa kwa kushambuliwa na wananchi wenye hasira kali, baada ya kudaiwa kupora Sh. milioni sita nyumbani kwa mfanyabiashara maarufu, Hussein Minja.

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Thomas Apson, alithibitisha kuwa mtu aliyeuawa kwa kipigo juzi usiku katikati ya Mji wa Mwanga, na kuwa ametambuliwa kwa jina moja la Tillya.

Apson aliieleza Nipashe kuwa mfungwa huyo akiwa na wenzake watatu, walivamia nyumbani kwa mfanyabiashara Minja maarufu kama ‘Hussein mafriji’ na kumtisha kwa mapanga kutoa fedha zote alizokusanya dukani kisha wakafanikiwa kuchukua Sh. milioni sita.

Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Salum Hamduni, alipotafutwa kueleza undani wa tukio hilo, alijibu kwa ujumbe mfupi wa maandishi ya simu ya mkononi (SMS) akisema: “Nipo nje ya ofisi yangu kwa sasa. Nikimaliza kikao nitakutafuta.”

Inadaiwa kuwa baada ya kupora fedha hizo ambazo ni mauzo ya vifaa vya kielekroniki katika duka lililopo mkabala na nyumba yake, watuhumiwa watatu wa ujambazi walifanikiwa kutoroka na Sh. milioni sita, lakini ‘Tillya’ alibaki na Sh. milioni sita, ambazo zilikamatwa alipouawa.

Kwa mujibu wa Apson: “Hao watu walikuwa wanne na huyo mfungwa aliyejulikana kwa jina moja la Tillya aliuawa na wananchi muda mfupi, baada ya kubaki kwa Hussein Mafriji, akimlazimisha aongeze pesa kwa sababu milioni sita haziwatoshi kugawana.

“Baada ya tukio hilo wananchi wenye hasira walimkamata na kumshushia kipigo hadi kupoteza maisha. Nimepewa taarifa kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama kwamba bado Polisi wanaendelea na uchunguzi kuhusu tukio hilo ili waweze kuwasaka na kuwakamata majambazi watatu waliotokomea na fedha hizo.”

Alisema baada ya Tillya na wenzake watatu kutekeleza tukio hilo la ujambazi, wananchi wenye hasira kali walimvamia na kuanza kumshambulia na kumuumiza vibaya.

"Askari Polisi waliokuwa doria na waliokuwa kituoni waliwahi katika tukio hilo na kufanikiwa kumuokoa Tillya asiendelee kushambuliwa, lakini alifariki muda mfupi,” alisema.

Akizungumza na Nipashe, Mfanyabiashara Minja alisema majira ya saa 3 usiku alitoa msikitini kuswali aliingia ndani akala chakula halafu akaingia bafuni kuoga.

“Nilifika chumbani nikawasha taa kisha nikaingia bafuni kwa ajili ya kuoga, nimetoka kuoga nashangaa taa ya chumbani imezimwa, na ghafla wakatokea watu wanne wakasema nipo chini ya ulinzi natakiwa kutoa fedha,” alisema.

“Walinipiga wakanikata sikio, kichwani na kunitoboa na bisibisi wakitaka nitoe fedha, nilitoa shilingi 12 wakagawana na mwisho wale watatu walitokea dirishani… walikokuwa wametoboa, akabaki mmoja ambaye ni kiongozi wao akitaka nitoe fedha zaidi nikamsihi aniache kwa kuwa sina fedha zaidi ya hizo,” alisema.

Minja alisema wakati wanamshambulia, alipigiwa simu na mmoja wa ndugu yake na aliiweka wazi huku akieleza amevamiwa na majambazi anahitaji msaada na ndipo polisi walijulishwa na huku wananchi wakianza kusogea eneo hilo, na kwamba jambazi huyo alivyotoka walimshambulia.

Habari Kubwa