Aliyebambikwa kesi ageuziwa kibao

20Mar 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Aliyebambikwa kesi ageuziwa kibao

JESHI la Polisi limesema linafanya uchunguzi dhidi ya mfanyabiashara Mussa Adam ambaye limebainika lilimbambika kesi ya mauaji.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Ahmed Msangi, picha mtandao

Limedai kuwa wakati linawachukulia hatua baadhi ya askari wakle walioshiriki kumbambika kesi, uchunguzi wa awali dhidi ya mfanyabiashara huyo umebaini ni mkora.

Wiki iliyopita, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ilieleza kuwa baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi mkoani Tabora walimbambika kesi ya mauaji mfanyabiashara huyo.


Akizungumza na Nipashe jana jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Ahmed Msangi, alidai mfanyabiashara huyo ni mkora.

Alidai alishafungwa miaka 20 jela kwa kosa la kubaka, alishaiba mahali na kukimbia na pingu na tukio la mwisho lililomfanya atiwe mbaroni na polisi na kubambikwa kesi ya mauaji, ni la wizi wa simu ya mwanamke kwenye kituo cha mabasi ambako alipigwa hadi kuvuliwa shati.

Msangi alidai mfanyabiashara huyo ni mtuhumiwa kama wengine, hivyo Jeshi la Polisi linamchunguza na akibainika kutenda kosa, atafikishwa mahakamani.

"Kilichoibuka hapa ni kitendo cha baadhi ya askari kumbambika kesi ambayo nayo tunachunguza ili nao wachukuliwe hatua," alisema.

Msangi aliongeza: "Lakini huyu mtuhumiwa naye ukweli ni kwamba siyo mtu safi, ni msumbufu kwenye jamii, ameshafanya matukio kadhaa.


"Pamoja na ukoera wake, polisi hawakutakiwa wafanye walichokifanya (kumbambika kesi ya mauaji). Walitaarifiwa kuwa kuna mtu amepigwa sana huko mtaani, walipofika walimkuta kweli akiwa katika hali mbaya, amepigwa hadi kavuliwa shati, kosa lilikuwa ni wizi wa simu ya mama mmoja, ambaye hata hivyo aliipata baada ya wananchi kumkamata mtuhumiwa.

"Bado ofisa wetu aliyetumwa kwenda Tabora kupeleleza tukio hili yuko huko anaendelea na kazi. Anapeleleza tukio la polisi waliodaiwa kumbambika kesi mtu huyu, lakini pia mtuhumiwa naye anachunguzwa kutokana na kosa au makosa yaliyomfikisha polisi, akibainika ameyatenda, atafikishwa mahakamani kama watu wengine."

Wiki iliyopita, Msangi akizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa taarifa za awali zimeonyesha mfanyabiashara huyo alionewa kubambikwa kesi ya mauaji na baadhi ya askari polisi.

Msangi alisema jeshi hilo lilipokea barua ya malalamiko kutoka kwa mfanyabiashara huyo ndipo Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai ilimtuma ofisa wake mwenye cheo cha juu kwenda Tabora kufanya uchunguzi.