Aliyefungwa maisha mhitimu Chuo Kikuu

24Nov 2016
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Aliyefungwa maisha mhitimu Chuo Kikuu

MFUNGWA anayetumikia kifungo cha maisha jela katika gereza la Butimba wilayani Nyamagana mkoani Mwanza, Machera Chacha (38), ni miongoni mwa wahitimu 4,038 wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) leo.

Atatunukiwa Stashahada ya Ualimu wa Shule ya Msingi.

Mfungwa huyo aliamua kujiendeleza kielimu ili awafundishe wenzake wanaofungwa wakiwa hawajui kusoma na kuandika, imeelezwa.

Mkurugenzi wa OUT tawi la Mwanza, Antyfrida Prosper, katika mazungumzo na Nipashe kwa simu jana, alisema Chacha ambaye alianza kutumikia kifungo chake mwaka 2008, alivutiwa kujiendeleza kimasomo baada ya kukutana na ofisa wa magereza aliyehitimu elimu ya juu katika chuo hicho.

Prosper alisema masomo ya mfungwa huyo yalikuwa yakitolewa gerezani na wakufunzi tofauti akiwamo yeye.

Alisema Chacha aliingia gerezani akiwa hajajiunga na chuo hicho lakini baada ya kukutana na ofisa huyo, alimsaidia kupeleka vyeti vyake katika chuo hicho na kuzijaza.

“Chacha ni miaka nane sasa tangu ahukumiwe, ni mwanafunzi wangu, alikuwa na nia ya kusoma na alipofika gerezani alitamani kusoma. Alipokutana na ofisa aliyehitimu OUT, alimwelezea nia yake ya kujiendeleza ingawa amefungwa maisha," alisema Prosper.

“Stashahada yake ina umuhimu akiwa gerezani, kuna watu ambao wanahukumiwa wa aina mbalimbali, wasiojua kusoma na kuandika, hata darasa la saba hawajahitimu wengine, hivyo Chacha alisema elimu yake itasaidia kuwafundisha wenzake.”

Alisema Chacha alipata mafunzo yake kwa mfumo wa ana kwa ana na kwamba pia alikuwa akipatiwa vitabu mbalimbali ili avisome akiwa gerezani.

“Akiwa gerezani anafundisha, anasema kufungwa siyo mwisho wa maisha, anafundisha wenzake kwa madaraja tofauti wanapangwa, wapo wanaoanza darasa la kwanza, wengine la nne, inategemeana.”

WAHITIMU WATATU
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Elifas Bisanda, alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa Chacha hatoweza kuudhuria katika mahafali hayo ya 31 yanayofanyika leo katika viwanja vya chuo hicho vilivyopo Bungo, Kibaha mkoani Pwani kutokana na kifungo chake.

Profesa Bisanda alisema mahafali ya mwaka huu ni ya kipekee kutokana na kuwa na wahitimu watatu wanaotoka katika makundi maalumu, akiwamo Chacha.

Alisema mbali na Chacha, wahitimu wengine kutoka makundi maalumu ni Dickie Mshana, mlemavu wa viungo anayetunukiwa shahada ya lugha na Adam Shabani, mwenye ulemavu wa kusikia ambaye atatunukiwa shahada ya elimu maalumu.

Katika hatua nyingine, Profesa Bisanda alisema idadi ya wahitimu katika chuo hicho imekuwa ikiongezeka kila mwaka na kufanya mpaka sasa wahitimu wote wa chuo hicho tangu kuanzishwa kufikia 30,788.

Alisema Tanzania inahitaji wataalamu wa fani mbalimbali wenye elimu ya juu, na kwamba idadi ya wahitimu nchini inatakiwa kuongezeka kutoka asilimia nne ya sasa mpaka 15.

“Tanzania itachukua zaidi ya miaka 10 hadi 20 ili kufikia kiwango cha asilimia 15 ya Watanzania wanaojiunga katika elimu ya vyuo vikuu nchini," alisema Profesa Bisanda.

"Kwa sasa ni asilimia nne pekee ya wanafunzi wanaojiunga vyuo vikuu, ikilinganishwa na idadi ya wahitimu kwa nchi kama ya Kenya.”

Aliongeza kuwa katika mahafali hayo ya leo, mgeni rasmi anayetarajia kuwatunuku walihitimu hao wa shahada ya uzamivu, uzamili, shahada ya awali, stashahada na astashahada ni Rais John Magufuli.

Habari Kubwa