Aliyehukumiwa kunyongwa aomba kuachiwa

15Jun 2019
Hellen Mwango
DAR
Nipashe
Aliyehukumiwa kunyongwa aomba kuachiwa

ALIYEKUWA Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni, (kwa sasa mkoa wa kipolisi Kinondoni), Mrakibu wa Polisi (SP) Christopher Bageni, aliyehukumiwa kunyongwa hadi kufa, ameiomba mahakama kumwachia huru kwa sababu uamuzi wa Mahakama ya Rufani Tanzania uliomtia hatiani haukumpa nafasi ya kujitetea.

Kadhalika, amedai kuwa uamuzi wa rufani iliyomtia hatiani iliyofunguliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ulikuwa na hoja za kisheria na kwamba hakupata nafasi ya kujibu na kujitetea.

Madai hayo yalitolewa jana na wakili wa mlalamikaji, Gaudiosis Ishengoma, wakati akiwasilisha hoja za mapitio mbele ya jopo la majaji watatu, likiongozwa na Jaji Stella Mugasha. Majaji wengine ni Ferdinand Wambari na Rehema Kerefu.

Ishengoma alidai kuwa maombi ya mlalamikaji dhidi ya DPP ni kuiomba mahakama kufanya mapitio ya uamuzi wake wa Septemba 16, 2016 uliomtia hatiani mteja wake.

Aidha, alidai kuwa uamuzi huo ulikuwa unalenga kutengua hukumu ya Mahakama Kuu iliyowaachia huru baada ya ushahidi wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha tuhuma za mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja.

Alidai kuwa pamoja na mambo mengine mamlaka ya mahakama hiyo ni kufanya mapitio uamuzi wake pale inapotokea ukiukwaji wa haki haiwezi kuachwa ikawa hivyo.

"Kwa uhalisia wa kesi hii rufani iliyoletwa na DPP, mlalamikaji hakupata nafasi ya kusikilizwa wakati Mahakama ya Rufani ilipotengua uamuzi wa kumtia hatiani, uamuzi huo wa Mahakama Kuu katika kutafsiri kifungu cha kanuni ya 22 na cha 23 ya adhabu kwamba huwezi kumtia hatiani mtu aliyesaidia kuua ukamwacha aliyeua," alidai na kuongeza.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya jopo na wakili wa mlalamikaji:

Jaji Wambari: Nini jukumu la Mahakama ya Rufani kusikiliza rufani?

Wakili: Mahakama ya Rufani ina kazi ya kupitia ushahidi kuona kama mahakama ya chini ilikwenda sawa katika kutoa hukumu yake. 

Jaji Wambari: Tusaidie mahakama ilisikiliza rufani na kuacha nini?

Wakili: Kuhusu kifungu cha 22 na 23 si sehemu ya hukumu. Watukufu majaji, hukumu ya mahakama kuu ilisema hakuna ushahidi kama watuhumiwa (mlalamikaji na wenzake ambao hawapo mahakamani), katika uamuzi wa rufani ya DPP Bageni hakusikilizwa na wala utetezi wake haukuzingatiwa katika rufani hiyo.

Akifafanua zaidi alidai kuwa Mahakama ilisikiliza ushahidi wa DPP ikaacha utetezi wa Bageni na kwamba ametiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu hiyo kwa ushahidi ambao haupo.

"Ukiangalia rufani ya DPP katika ushahidi wa mashahidi 37 wa Jamhuri na 13, wa utetezi hakuna ushahidi uliomgusa Bageni, mahakama hii ilipomtia hatiani imepoteza haki yake naiomba mahakama isiruhusu tena ukiukwaji huu wa haki," alidai Ishengoma wakati akihitimisha hoja za maombi ya mlalamikaji.

Upande wa mlalamikiwa DPP ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ladislaus Komanya, ulidai kuwa mlalamikaji hana sababu za msingi za kutengua uamuzi uliomtia hatiani.

Komanya alidai kuwa rufani ya kesi hiyo ilishasikilizwa kwamba sasa si wakati wake kusikilizwa kwa mgongo wa mapitio. Alidai kuwa Bageni alipata nafasi ya kusikilizwa na kwamba mahakama itupilie mbali mapitio hayo.

"Mahakama hii ina uwezo wa kusikiliza jambo na kulifanyia uamuzi kwa hiyo mambo yatakayoletwa yazingatie kifungu cha 66 kidogo cha (1) (b) cha kanuni ya adhabu, maombi ya mlalamikaji tunaona hayajakidhi vigezo vinavyotakiwa, kwa kuruhusu maombi kama haya ambayo hayafiki mwisho tunafungua mwanya kwa wengine yatupiliwe mbali," alidai Komanya.

Ishengoma alikijibu hoja za mlalamikiwa alidai kuwa si sahihi na kwamba kifungu cha 66 (1) (b) hakijakidhi vigezo vya kupiga mapitio hayo na kwamba mtuhumiwa kama Bageni ambaye alitiwa hatiani na Mahakama ya Rufani na hana kwingine kwa kukimbilia kudai haki yake.

Alidai kuwa mapitio haya ni tofauti na mengine ambayo mtuhumiwa ametiwa hatiani na Mahakama ya chini.

Aidha, jopo hilo lilisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili mahakama inakwenda kuzifanyia kazi na pande hizo zitajulishwa tarehe ya uamuzi.

Katika maombi yake SP Bageni anapinga hukumu iliyotolewa katika mahakama hiyo chini ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Bernard Luanda, Sauda Mjasiri na Senistocles Kaijage kwamba lilifanya makosa ya dhahiri.

Pia, anadai kuwa jopo hilo lilifanya makosa katika mwonekano na kusababisha haki kutokuzingatiwa mahakama hiyo itenguwe hukumu hiyo.

Habari Kubwa