Aliyekuwa RC Manyara Joel Bendera kuzikwa Jumapili wilayani Korogwe

07Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Aliyekuwa RC Manyara Joel Bendera kuzikwa Jumapili wilayani Korogwe

Mwili wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Nkaya Bendera aliyekutwa na mauti jana katika hospitali ya taifa Muhimbili unatarajiwa kuzikwa Jumapili katika eneo la Manundu wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.

Akizungumza na ITV nyumbani kwa marehemu Sinza jijini Dar es Salaam unapofanyika msiba, mdogo wa marehemu Allan Michael Bendera amesema taratibu za mazishi zinaendelea na mwili wa marehemu ambaye alikuwa akisumbuliwa na sukari utaagwa jumamosi katika hospitali Jeshi ya Lugalo na wadau mbalimbali saa nne asubuhi.

MAREHEMU JOEL BENDERA

Wakizungumza na ITV viongozi na watu wa karibu na marehemu wamesema kuwa kifo hicho ni pigo kwa taifa kumpoteza mtu mchapakazi na mwenye kujituma ambaye siku zote alikuwa nguzo ya maendeleo katika jamii.

Marehemu Joel Bendera ameacha mke na watoto watatu na atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa alioutoa kwa serikali na jamii kwa ujumla katika idara mbalimbali alizofanyia kazi pamoja na mchango wake mkubwa katika tasnia ya michezo.

Habari Kubwa