Aliyenusurika ajali boti arukwa akili

12Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Aliyenusurika ajali boti arukwa akili

MMOJA wa manusura 33 wa ajali ya boti iliyozama Bahari ya Hindi na kusababisha vifo vya watu 13, amebainika kurukwa na akili na matabibu wa Hospitali ya Rufani ya Tanga wanaomtibu.

Juzi alfajiri, boti ya Burudan, maarufu Sayari, yenye namba za usajili MV 25512, mali ya Suleiman Vuai, mkazi wa Pemba, ilizama karibu na Kisiwa cha Jambe ilipokuwa inatoka bandari bubu ya Sahare jijini Tanga kwenda Pemba ikiwa na shehena ya chakula, bia na abiria zaidi ya 40.

Katika ajali hiyo, watoto sita walikuwa miongoni mwa watu 12 waliopoteza maisha huku 33 wakiokolewa na wavuvi wakiwa hai na kukimbizwa kwenye hospitali hiyo, maarufu Bombo.

Hata hivyo, jana jioni Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali hiyo, Dk. Goodluck Mbwilo, aliiambia Nipashe jijini humu kuwa majira ya
saa 10 alasiri walipokea maiti ya mtoto mwenye umri kati ya miaka mitano na sita ikiwa imeharibika.

Hadi jana saa 9:38 alasiri, manusura 32 walikuwa wameruhusiwa kuondoka hospitalini hapo huku msichana mmoja mwenye umri wa miaka 12 akishindwa kuruhusiwa kutokana na kurukwa akili.

Msichana huyo (jina tunalihifadhi) amebainika kurukwa na akili kutokana na ajali hiyo ambacho taarifa za awali zinadai ni mawimbi makali yaliyopiga boti hiyo na kusababisha maji kuingia ndani.

Akizungumza na Nipeshe jijini humu jana, Dk. Mbwilo, alisema majeruhi huyo aliyerukwa na akili yupo chini ya uangalizi wa madaktari bingwa.

"Mgonjwa huyu anaonekana karukwa na akili kutokana na kwamba hawezi kuzungumza kitu chochote na amekuwa kama bubu. Madaktrai wanaendelea kupambana kuhakikisha wanamrejesha katika hali ya kawaida," alisema.

Aliongeza kuwa miili ya maiti 12 iliyokuwa imehifadhiwa hospitalini hapo ilitambuliwa na kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maziko.

Aliwataja waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni Halima Songoro (29, mkazi wa Muheza, Tanga), Mwanashari (Mpemba aliyekuwa anaishi Chongoleani, Tanga), Yusuph Maoud (3, mkazi wa Pemba), Ally Masoud Abdallah (5, mkazi wa Pemba), Muhidini Mahabani (23, mkazi wa Mikanjuni Chakechake, Pemba), Fatuma Abdi Kombo (6, mkazi wa Msakangoto, Tanga) na Hadija Abdi Kombo (2 Msakangoto).

Wengine ni nahodha wa boti, Badru Saidi (60, mkazi wa Pemba), Asha Ayubu (40, mkazi wa Pemba), Mudi Mrisho (20, mkazi wa Mkuzi, Muheza), Murhati Mkubwa (5, mkazi wa Magaoni, Tanga) na Mariam Shariff (mkazi wa kata Chongoleani, Tanga).

SUMATRA
Kutokana na ajali hiyo, Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) mkoani humu imepiga marufuku usafirishaji wa abiria kwa kutumia majahazi na boti ambazo hazijaidhinishwa kwa ajili hiyo.

Ofisa Mfawidhi wa Sumatra mkoani humu, Dk. Walukani Luhamba, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa majahazi mengi ambayo yanafanya safari zake kati ya Tanga na Pemba hajasajiliwa kubeba abiria hivyo kufanya hiyo ni kinyume cha utaratibu na ni hatari kwa maisha ya watumiaji wake.

Dk. Walukani alisema ajali hiyo ilisababishwa na upepo mkali uliosababisha baadhi ya mbao kung’oka katika jahazi hilo na kupelekea maji kujaa na kusababisha maafa hayo

Alisema wananchi wengi wamekuwa na mazoea ya kuzitumia bandari bubu zilizopo katika Mkoa wa Tanga kusafirishia bidhaa mbalimbali huku majahazi hayo yakitumika pia kubeba abiria kinyume cha sheria.

Mkaguzi wa Sumatra Mkoa wa Tanga, Christopher Mlelwa, alisema mkoa unakadiriwa kuwa na bandari bubu 45 ambazo kisheria ni vituo vya uvuvi na vinatakiwa kujishughulisha na shughuli zitokanazo na mazao ya baharini na si vinginevyo.

Mlelwa alisema bandari zilizo rasmi ni Bandari za Tanga na Pangani na kwamba vituo vingine vyote vimeandaliwa kwa ajili ya shughuli za uvuvi, hivyo kuendesha shughuli za usafirishaji wa abiria na mizigo ni kwenda kinyume cha taratibu zilizowekwa na mamlaka husika.

Alisema mmiliki wa boti iliyozama, Vuai bado hajakamatwa, lakini akabainisha kuwa wamekabidhi jukumu hilo kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga kufanya upelelezi wake kubaini kwanini alivunja sheria za Sumatra.

Habari Kubwa