Aliyeongoza kitaifa aanika siri mafanikio

16Jan 2022
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Aliyeongoza kitaifa aanika siri mafanikio

MTAHINIWA wa kidato cha nne kutoka Shule ya Sekondari St. Francis Girls, Consolata Lubuva, aliyeongoza kitaifa kwenye matokeo ya kitaifa mwaka 2021, ametaja siri ya mafanikio yake pamoja na ndoto yake.

Shule ya Sekondari St. Francis Girls, Consolata Lubuva.

Akizungumza na Nipashe nyumbani kwao Salasala mkoani Dar es Salaam, Consolata alisema amepokea kwa furaha matokeo hayo kwa kuwa matarajio yake yalikuwa ya wastani lakini amefanya viruzi.

"Siri ya mafanikio haya ni Mungu. Nilikabidhi masomo haya kwa Mungu naye amenisaidia. Wazazi wamekuwa msaada mkubwa kwangu pia wamekuwa mfano mzuri sana. Mfano mama yangu ni daktari wa falsafa amenihamasisha sana," alisema Consolata na kuongeza;

"Pia nilijitahidi kupanga muda wangu vizuri, nilihakikisha nina muda wa kusoma, kusali na kufanya mambo muhimu ya shule. Haya ndiyo yalinipa mafanikio."

Alisema ataongeza juhudi zaidi ili afikie ndoto yake ya kuwa daktari wa watoto.

Consolata alitaja mambo yaliyomwezesha kuongoza katika mtihani huo ni kusoma kwa bidii na kufanya maombi na kwamba wakati matokeo hayo yanatangazwa, alikuwa akisikiliza nyimbo za injili nyumbani kwao, Salasala.

"Nilikuwa natarajia kuwa naweza kuingia kwenye kumi bora kitaifa lakini si kuongoza kwa kuwa namba moja," alisema Consolata.

Alisema wakati akifanya mtihani, somo pekee lililomsumbua ni Fizikia, lakini mengine hayakuwa tatizo kiasi cha kumpa ujasiri kuwa angefaulu mitihani yake ya kidato cha nne.

 Mama wa mwanafunzi huyo, Beatrice Halii, alisema wanamshukuru Mungu amewapa kicheko kupitia mtoto wao na kwamba uwezo wake ulijulikana akiwa darasa la kwanza na walimwendeleza kwa bidii hadi sasa imedhihirika.

Mama huyo aliwashauri wazazi kutambua karama za watoto na kuzilea, huku akieleza kuwa mtoto wao alikuwa akiomba zawadi ya kitabu cha masomo wakati wote.

Katika matokeo ya mtihani huo yaliyotangazwa jana na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA),Consolata ndiye mwanafunzi aliyefaulu vizuri zaidi kati ya wanafunzi 483,820 waliofanya mtihani huo mwishoni mwa mwaka jana.

Alisema Binti yake alikuwa akijituma kwa kupanga muda wa kazi za nyumbani na za shule bila kukumbushwa na mtu yoyote.

VINARA WENGINE

Nipashe ilifika katika Shule ya Sekondari St. Francis na kukutana baadhi ya wanafunzi waliofanya vizuri akiwemo Bhutoi Nkangaza aliyeshika nafasi ya pili kitaifa na Glory Mbele ambaye ameshika nafasi ya nne.

Wanafunzi hao walitaja sababu mbalimbali zilizowafanya wang’are kwenye matokeo hayo kitaifa na kuifanya shule yao ishike nafasi ya pili kitaifa.

Bhutoi alisema wakati matokeo yanatangazwa alikuwa yupo nyumbani kwao na alikuwa hana taarifa yoyote na alipigiwa simu na wenzake lakini bado hakuamini.

Alisema alipofika nje alimkuta mama yake akiwa analia kwa furaha na ndipo akaamini kuwa alichoambiwa na wenzake ni kweli na kwamba alianza kupokea simu nyingi za kumpongeza.

Siri ya mafanikio yake, alisema ni kusoma kwa bidii, kumuomba Mungu pamoja na ushirikiano mzuri baina ya wanafunzi hao akidai kuwa walikuwa wanasaidiana kwenye maeneo ambayo walikuwa wanaamini kuwa ni magumu.

Hata hivyo Bhutoi ambaye ana ndoto ya kuwa daktari wa watoto aliwataka wanafunzi wengine waliobaki shuleni hapo kusoma kwa bidii ili na wao wafikie mafanikio waliyoyafikia wao, huku akiwashukuru walimu na wazazi kwa kuwasaidia.

Naye Glory ambaye ameshika nafasi ya nne kitaifa alisema mazingira ya shule yao yanavutia wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kwamba pia walimu wa shule hiyo wanawafundisha kujitambua kuanzia hatua za mwanzo wanapojiunga kidato cha kwanza.

Mwalimu wa Taaluma wa shule hiyo, Reginald Chiwangu, alisema mbali na shule hiyo kushika nafasi ya pili kitaifa lakini ndiyo iliyoongoza kwenye somo la Jiografia ambalo anafundisha yeye.

Alisema wamekuwa wakiwaelekeza zaidi wanafunzi kutambua malengo yao ya kwenda shuleni hapo kuliko kuwafundisha kwa kuwapa adhabu zikiwamo za viboko.

Imeandaliwa na Mary Geofrey, Salome Kitomari (Dar) Nerbart Msokwa (Mbeya).

Habari Kubwa