Aliyepata ajali gari la RC afariki dunia

07Aug 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Aliyepata ajali gari la RC afariki dunia

KASOBI Shida (26), mtoto wa dereva wa Mkuu wa Mkoa wa Mara aliyepata ajali akiendesha gari linalotumiwa na baba yake, Shida Masaba (55) kumwendesha mkuu wa mkoa huo, amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu kutokana na ajali hiyo.

Ajali hiyo ilitokea Jumapili baada ya baba wa kijana huyo kurejea nyumbani akitumia gari hilo aina ya Land Cruiser lenye namba za usajili STL 5961 na Kasobi kulichukua na kuondoka nalo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Juma Ndaki, aliliambia Nipashe jana kuwa kijana huyo, alifariki dunia usiku wa kuamkia jana.

Alisema baada ya ajali hiyo, Kasobi alilazwa katika Hospitali ya Rufani ya Musoma akiendelea na matibabu ya majeraha aliyopata.Alisema taratibu za mazishi zinafanywa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Kamanda Ndaki aliongeza kuwa baada ya ajali hiyo, baba wa kijana huyo, Masaba alipata mshtuko na kulazwa hospitalini na hadi kifo cha mwanawe kinatokea, alikuwa hajaruhusiwa kwenda nyumbani.