Aliyerejeshwa na NEC Dar atamba ushindi bila kampeni

24Sep 2020
Christina Mwakangale
Dar es Salaam
Nipashe
Aliyerejeshwa na NEC Dar atamba ushindi bila kampeni

MGOMBEA ubunge Jimbo la Ubungo kupitia CHADEMA, Boniface Jacob, amesema maisha yake kwa wananchi wa jimbo hilo, yanatosha kuchaguliwa kuwa mbunge, bila kutegemea kampeni.

Amesema pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kumrejesha kugombea kiti cha jimbo hilo, licha ya wagombea wa vyama vingine kuanza kufanya kampeni wiki tatu kabla yake, hata akifanya kampeni siku moja atachaguliwa na wananchi.

Boniface aliyasema hayo jana akizungumza na Nipashe kuelezea namna atavyoweza kufidia siku alizozuiwa kugombea, baada ya Agosti 29, mwaka huu, kupokea barua ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ubungo, kumuengua kugombea ubunge jimbo hilo.

“Maisha yangu yenyewe tosha tu, ni kampeni hata ningezuiwa, ingeachwa siku moja, bado wananchi wa Ubungo wanahitaji tu kujua nagombea basi. Kwa hiyo ‘issue’ ya kampeni sio kitu,” alisema.

Kwa siku nilizorudi tayari nimekamilisha mzunguko wa awamu ya kwanza, nilianza Mabibo, Makurumla, Manzese na Kimara, Sinza, leo (jana) namalizia Makuburi kata ya nane, leo (jana) naanza raundi ya pili,” alisema Boniface.

Alisema wananchi wa jimbo hilo, wanafahamu utendaji kazi wake tangu akiwa diwani na hatimaye mbunge.

“Wakinichagua miradi niliyoianza tutaimalizia, vitu ambavyo nimefanya katika jimbo hilo kama shule, zahanati na barabara ni alama ambazo nimeziacha, kila kata nilizunguka na kushiriki kuleta maendeleo,” alisema Boniface ambaye aliwahi kuwa meya wa Ubungo.

Agosti 29, mwaka huu, katika ukurasa wake wa twitter, Boniface aliandika: Nimepokea barua kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Ubungo kuenguliwa kugombea ubunge.”
Septemba, mwaka huu, NEC ilikubali rufani 13 na kuwarejesha katika orodha ya wagombea ubunge 13 baada ya kupitia nyaraka walizowasilisha.

Kati ya rufani hizo ni kutoka majimbo ya Singida Magharibi, Madaba, Ilemela, Namtumbo, Bagamoyo, Liwale, Tunduma, Bukene, Ubungo na Kigamboni.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Charles Mahera, ilisema kuwa Tume imechambua vielelezo, nyaraka na maelezo ya warufani na warufaniwa yaliyowasilishwa, ili kuhakikisha inatenda haki wa mujibu wa sheria.

Habari Kubwa