Aliyetaka marehemu asizikwe hadi alipe ng’ombe kukamatwa

12Apr 2017
John Ngunge
ARUSHA
Nipashe
Aliyetaka marehemu asizikwe hadi alipe ng’ombe kukamatwa

KIONGOZI wa kimila wa kijiji cha Endagulda, Joseph Daniel, aliyeamuru ndugu wa marehemu asizikwe hadi walipe faini ya ng’ombe baada ya kutengwa na jamii, ametakiwa kukamatwa na kufunguliwa mashtaka.

Alitoa agizo hilo kwenye kijiji hicho baada ya baadhi ya wananchi kumlalamikia mzee wa kimila Joseph Daniel, kuagiza marehemu huyo asizikwe mpaka apigwe faini ya ng’ombe mmoja.

Inadaiwa Boay Gadii (42), aliuawa kwa kukatwa na mapanga na watu wasiojulikana baada ya kuibiwa ng’ombe wake 50 aliokuwa akiwafuga kwenye kijiji hicho.

Akizungumzia kuhusu hilo, Mofuga alisema haiwezekani viongozi wa kimila kujiamulia mambo yao ya kisheria ambayo yanayapingana na sheria za nchi kwa kuwa hali hiyo ikiachiwa italeta uvunjifu wa amani.

“Sheria za kimila tunataka ziwe rafiki na sheria za nchi, hatujakataa mila, desturi wala utamaduni, lakini hizi sheria kandamizi za kunyanyasa watu sizitaki hapa,” alisema.

Alisema mzee huyo aliyeagiza maiti ipigwe faini ndipo azikwe, anatakiwa kukamatwa mara moja na kufikishwa mahakamani ili vitendo kama hivyo visirudiwe tena.

Alimuagiza Mkuu wa Polisi wa Mbulu, kuwakamata watu wanaodaiwa kumuua Gadii na kisha kuiba ng’ombe wake 50 na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.

Hata hivyo, mzee huyo wa kimila Daniel alisema, alitekeleza maazimio ya wazee wa kimila walioamua kuwa Gadii atengwe na jamii kutokana na vitendo vyake.

“Hili suala tuliliamua kwenye vikao vyetu vya kimila hivyo sikuamua peke yangu, ni wazee wa kimila ndiyo waliomtoa adhabu hii kwa Gadii,” alisema.

Hata hivyo, marehemu alizikwa baada ya ndugu zake kulipa ng’ombe mmoja dume.

Kwa upande wao, wakazi wa kijiji cha Endagulda walisema vitendo vinavyofanywa na wazee wa kimila ni vya kibabe ambavyo haviko kisheria.

Richard Songay, alisema mkuu wa wilaya amefanya jambo muhimu kukemea tabia kama hizo zinazolalamikiwa na baadhi ya viongozi wa kimila kwa muda mrefu.

Habari Kubwa