Amani, amani uchaguzi mkuu 2020

23Oct 2020
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe
Amani, amani uchaguzi mkuu 2020

Wananchi, viongozi wa madhehebu ya dini na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa wameombwa kuitunza, kuilinda na kuienzi amani ya nchi katika kipindi chote kabla na baada ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28,2020.

Hayo yamesemwa leo na Msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Ilemela John Wanga wakati wa zoezi la kuwaapisha wagombea ubunge na mawakala wao.

Amesema vyama saba ambavyo ni CCM, ADC, ACT -Wazalendo, CHADEMA,DP, DEMOKRASIA MAKINI na NRA ndivyo vilivyokidhi masharti ya uteuzi na ndio wataapishwa ili wapate fursa ya kuingia kwenye vituo vya majumuisho ya kura za rais,ubunge na madiwani kwa ngazi ya kata.

"Jimbo lina jumla ya vituo vya kupigia kura 795 vilivyotawanyika katika kata 19, vituo hivyo vina jumla ya wapiga kura 302,589 walioandikishwa kwenye daktari la kudumu la wapiga kura hivyo uchaguzi utakapofanyika kwa amani ndio msingi wa kufanya maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa" amesema  Wanga.

Ameongeza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeleta vifaa mbalimbali vya uchaguzi ambavyo vimefikia asilimia 90  katika jimbo hilo hivyo uchaguzi utafanyika kwa ufanisi kadri ilivyopangwa.

Sambamba na hayo alitoa wito kwa wananchi wote wa jimbo hilo waliojiandikisha katika daftari la wapiga kura wajitokeze kwa wingi Oktoba 28 mwaka huu ambapo vituo vya kupigia kura vitafunguliwa saa moja asubuhi na kufungwa Saa 12 kamili jioni. 

Habari Kubwa