Amber Rutty, mpenzi wake na 'James Delicious' jela miaka 5

25Sep 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Amber Rutty, mpenzi wake na 'James Delicious' jela miaka 5

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu Msanii Rutyfiya Abubakary maarufu kama 'Amber Rutty' na mpenzi wake Said Bakary na James Charles (James Delicious) kulipa faini ya Mil. 11 ama jela miaka 5 baada ya kutiwa hatiani kwa makosa matatu ikiwemo kufanya mapenzi kinyume na maumbile.

Msanii Rutyfiya Abubakary maarufu kama 'Amber Rutty' na mpenzi wake Said Bakary na James Charles (James Delicious) wakiwa mahakamani. picha mitandao.

Hata hivyo watu hao wameshindwa kulipa faini hiyo kwa leo, hivyo wamepelekwa Gerezani.

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya baada ya mahakama hiyo kujiridhisha pasina kuacha kwa ushahidi uliotolewa na Upande wa Mashitaka.

"Nimezingatia hoja za pande zote mbili na athari za makosa haya, ni kweli washitakiwa wote vijana na wanategemewa, nimeona mshitakiwa wa kwanza anajutia. 

Mshitakiwa wa Kwanza, Pili na Tatu ni wakosaji wa kwanza, kutokana na mazingira ya kesi hii adhabu yake ni miaka 30 kila kosa ambapo nikiwafunga mtapotea kabisa,"

"Hivyo kwa mazingira mliyoyasema na lengo la adhabu ni kujirudi, mshitakiwa wa kwanza utalipa Milioni 3 ama jela miaka 5,  mshitakiwa wa Pili utalipa faini ya Milioni 3 ama jela miaka 5 na mshitakiwa wa tatu faini Milioni 5 ama jela miaka 5 adhabu zitaenda sambamba," amesema.

Awali kabla ya adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Faraja Nguka  aliieleza mahakama kwamba "Hakuna rekodi za makosa ya nyuma, pia kutokana na makosa waliyotiwa nayo hatiani ni makosa ambayo yamezuiliwa hata na vitabu vitukufu na yakiwa na madhara makubwa kwa jamii na hayana tiba, tunaomba iwape adhabu stahiki ili iwe fundisho,".

Katika utetezi wao, Amberutty alisema kwamba; "Naiomba mahakaka inipunguzie adhabu nina watoto wananitegemea, mmoja ana matatizo ya Pumu, pia nina wazazi wangu wananitegemea, pia nina maradhi ya TB yananisumbua,"

Naye mshitakiwa Said Bakary alieleza kuwa; "Naiomba mahakaka isinipe adhabu kali mimi ni mtoto mkubwa ninayetegemea kwa familia ya watoto watatu, mama yangu amezeeka na ninasumbuliwa na TB natumia vidonge, mahakama inionee huruma,"

Pia mshitakiwa James kupitia Wakili wake alisema; "Naomba mahakama itoe adhabu ndogo kwa sababu haijawahi kutiwa hatiani wala rekodi ya jinai. Pia alionyesha ushirikiano tangu shauri lilipofunguliwa Mahakamani. Pia ni mtu aliyeonyesha utii na wito uliotolewa na RC aliutii na kufika Polisi. Pia mshitakiwa ni kijana mwenye umri mdogo familia yake inamtegemea, pia ana mzazi mmoja".

Katika hukumu hiyo, Hakimu Isaya amesema upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi 10, huku upande wa utetezi wakijitetea washitakiwa wenyewe.

Amesema katika hukumu hiyo hoja kuu zilikuwa 7 ikiwemo kama mshitakiwa Amber Rutty ndiye aliyeonekana katika video ya ngono ama lah, pia kama mshitakiwa huyo ameingiliwa kinyume na maumbile ama lah, pia kama mshitakiwa Said alimuingilia kinyume Amber Rutty.

Hakimu Isaya amesema kuwa baadhi ya hoja hazikuwa na shaka ikiwemo iliyomuhusu mshitakiwa Amberutty ambaye alipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili na kufanyiwa vipimo sehemu ya nyuma na kubaini kupo wazi.

Katika kesi hiyo kosa la kufanya mapenzi kinyume na maumbile lilikuwa linamkabili Amber Rutty, ambapo anadaiwa amelitenda kati ama baada ya October 25, 2018 ambapo alimruhusu Said Bakary kumuingilia kinyume na maumbile, kosa ambalo amelikana.

Pia kosa jingine la kufanya mapenzi kinyume na maumbile, linamkabili mshtakiwa wa pili Said Bakary ambapo anadaiwa kati ama baada ya October 25,2018 jijini Dar es Salaam alifanya mapenzi na Amber Rutty kinyume na maumbile ambapo alisema si kweli.

Kosa la tatu la kuchapisha video ama picha za ngono, ambapo linamkabili James Charles ama James Delicious akidaiwa kati ya October 25,2018 alisambaza video za ngono kupitia magroup ya Whatsapp.

Habari Kubwa