Amchoma moto mwanawe madai wizi ugali nyama

21Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
MTWARA
Nipashe
Amchoma moto mwanawe madai wizi ugali nyama

JESHI la Polisi mkoani Mtwara, linamshikilia Muwaza Abeid (29) kwa tuhuma za kumchoma moto na kumjeruhi mwanaye mwenye umri wa miaka minane ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili Shule ya Msingi Naliendele, kwa madai ya kuiba ugali nyama wa bibi yake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Mark Njelwa.

Akizungumza na Nipashe jana kwa simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Mark Njelwa, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba mama huyo anashikiliwa kwa ajili ya kuhojiwa kabla ya sheria kuchukua mkondo wake.

“Hili tukio ni kweli limetokea mtoto amejeruhiwa kwa kuchomwa moto vibaya mkono wa kulia na mama yake mzazi kisa alidai kaiba ugali nyama ulioachwa kwa ajili ya bibi yake,” alisema.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana mkoani humo zilizothibitishwa na Ofisa Ufuatiliaji na Tathimini wa Kituo cha Msaada wa Sheria Manispaa ya Mtwara Mikindani, Judith Chitanda, tukio hilo lilitokea Julai 3, mwaka huu, na mama yake kumficha ndani huku akimtibu kienyeji.

Alisema baada ya kumhoji alisema mwanawe huyo alikula ugali na nyama ambao ulikuwa amewekewa bibi yake aliyekuwa amekwenda shambani.

Kwa mujibu wa ofisa huyo, bibi aliporudi alimwuliza mtoto huyo kama amekula hicho chakula na alikiri kula, lakini mama yake alimfunga mikono yote miwili kwa kutumia majani ya mnazi huku akimtisha.

Alisema mtoto huyo aliangukia eneo lenye moto na majani hayo kushika moto na kumuunguza mkono wa kulia.

“Muda mwingi mama yake alikuwa analia kujutia tukio hilo. Anaomba jamii imsamehe na hakutegemea mwanawe anaweza kuungua kwa kiasi hicho na kwamba ni mtundu kwa kuwa amekuwa na tabia ya udokozi hadi fedha na siku hiyo alitoka kwa shangazi akiwa ameshakula chakula cha mchana lakini kutokana na udokozi akala chakula cha bibi yake,” alisema.

Kamanda Njelwa alisema mtoto huyo anaendelea na matibabu hospitalini.

Habari Kubwa