AMDT yasisitiza Watanzania kufanya kilimo chenye tija

08Dec 2023
Maulid Mmbaga
DAR ES SALAAM
Nipashe
AMDT yasisitiza Watanzania kufanya kilimo chenye tija

TAASISI ya Kuboresha Mifumo ya Masoko ya Kilimo Tanzania (AMDT) imeendelea kuhamasisha Watanzania kufanya kilimo chenye tija kwa kutumia mbegu zilizo boreshwa zikiwemo za Alizeti, jamii ya mikunde na Mahindi ili kuongeza mnyororo wa thamani.

Hayo yamesisitizwa leo mkoani Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa AMDT, Charles Ogutu, wakati akifungua mafunzo kwa wanahabari ambayo yanalenga kuwaongezea uelewa juu ya masuala yanayohusu kazi zinazofanywa na taasisi hiyo pamoja na yanayohusu kilimo bora ili waweze kuitumia kuelimisha jamii kupitia taarifa mbalimbali.

Amesema sababu kubwa ya kuanzishwa kwa taasisi hiyo ilikuwa ni kutatua changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikijirudia, akieleza kwamba viongozi wa kisiasa na wadau wa maendeleo wamefanya jitihada nyingi kwenye sekta ya kilimo ili kuzitatua.

“Pamoja na jitihada hizo mabadiliko bado hayajawa makubwa kama tunavyotarajia au tungetamani kuwa yawepo, hivyo ikaonekana haja ya kuanzisha taasisi ambayo itatumia mfumo kuangalia matatizo ya kimfumo ambayo yakitatuliwa yanaweza kutupeleka katika mabadiliko ya kweli wanayoyatarajia kwenye sekta ya kilimo,” amesema Ogutu.

Ameongeza kuwa jitihada hizo zinazofanyika kwenye kilimo ni kwasababu ndiyo sekta Mama inayotegemewa karibu na kila taifa, na kwamba takwimu zinaonyesha kuwa sekta hiyo inachangia ajira takribani asilimia 65.

Aidha, amesema AMDT katika utendaji wao wamejigawa katika misingi miwili, ikiwemo utekelezaji ambako wanachagua mazao ambayo wanaona yanaumuhimu zaidi na kutafuta changamoto za kimfumo na kuona ni namna gani wanaweza kushirikiana na wadau wengine kuzitatua.

Amesema nguzo ya pili ya AMDT ni kuangalia namna gani changamoto hizo zikisha tatuliwa zinaweza kuwafikia watu wengi zaidi, akieleza kuwa wamekuwa wakijihusisha zaidi na zao la Alizeti, jamii ya mikunde na mahindi.

“Mazao haya yana umuhimu wa kipekee na waziri mwenye dhamana amekuwa akizungumzia ajenda hiyo kila wakati kwamba ifikapo 2030 tunataka sekta ya kilimo iwe imekuwa kwa asilimia 10, ndio ndoto ya waziri na Rais ameliafiki hilo,” amesema Ogutu.

Pia amesema programu mbalimbali zinazofanyika kama Jenga Kesho Bora (BBT) ni kujaribu kuhakikisha kwamba ifikapo 2030 sekta ya kilimo inatoka kwenye ukuaji wa asilimia nne hadi 10, na kwamba wizara ilifanya tafiti kuwa ni mazao gani yakitiliwa msisitizo yatasaidia kufikia malengo hayo wakabaini kwamba ni ya nafaka, mafuta ya kupikia na jamii ya mikunde.

Hata hivyo ameeleza kuwa ajenda hiyo ilikuja wakati ambao AMDT ilishaanza kabla, na kwamba bahati nzuri baadhi ya mazao hayo niya kimkakati na yako kwenye Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (SDPll).

Vile vile ameeleza kuwa katika mazao hayo alizeti imeorozeshwa kama zao muhimu ambalo linaweza kulisaidia taifa katika kupunguza gharama ya kuangiza mafuta ya kula kutoka nje, na kwamba mengine yote wanayoshughulika nayo yako kwenye mkakati wa serikali.