Amref yasaidia wajasiriamali wa usafi wa mazingira Nyamagana Ilemela

07Aug 2020
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe
Amref yasaidia wajasiriamali wa usafi wa mazingira Nyamagana Ilemela

Amref Tanzania ikishirikiana na Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, imeanzisha mradi wa kuboresha usafi wa mazingira kwa watu wenye kipato cha chini kibiashara jijini humo kupitia msaada wa kifedha kutoka jiji la Madrid nchini Hispania.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Shirika la Amref  Health Africa nchini Tanzania, Meneja wa Miradi ya Usafi na Mazingira,  Mhandisi Mturi James, alisema lengo la mradi ni kusaidia juhudi za Serikali kuongeza na kuboresha huduma za usafi wa mazingira kupitia kamapeni ya kitaifa NSC-II (2016-2020).

Katika tukio hilo Mhandisi James alikabidhi bajaji nne zenye thamani ya milioni 30 kwa vikundi vinavyojihusisha na ujasiliamali wa usafi wa mazingira, ili kuendeleza shughul zao za mradi. 

Akizungumza katika tukio hilo, alisema ili kufikia mkakakati wa Kitaifa wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini (MKUKUTA-2015) na kufikia Malengo Endelevu ya Millenia (SDGs-2030), mradi huo unatoa mafunzo ya ujasiriamali wa usafi wa mazingira na kuwapatia vitendea kazi (bajaji) ili waweze kutoa huduma za kuzoa na kusafirisha taka hadi kwenye vituo vya kuchakata taka.

"Lengo lingine ni kuwawezesha na kuwanufaisha  akina mama na vijana katika maeneo ya wakazi wenye kipato cha chini kwa kuwezesha kupata fursa za kuongeza kipato na kuwakuza kiuchumi kwa kufanya ujasiriamali wa kuzalisha bidhaa mbadala kutokana na taka ngumu na taka vinyesi ili kurahisisha zoezi la uchakataji wa taka hizo kwa ajili ya kutengeneza mkaa mbadala, mbolea na gesi pia mradi huu utachangia utekelezaji wa mpango mkakati wa jiji la Mwanza wa mwaka 2004 wa kusimamia taka ngumu na kuboresha vyoo"alisema James.

Aliongeza wataongeza fursa kwa jamii nzima katika uelewa na mahitaji ya kusimamia na kuondoa taka katika maeneo ya makazi,kutoa kutoa elimu ya ujenzi wa vyoo bora na huduma za kuondoa vinyesi katika ngazi ya kaya, sambamba na ukiijengea Serikali uwezo wa kutoa huduma kwa kushirikiana na taasisi binafsi na wananchi kupitia mbinu za kibiashara ,hivyo mradi huo kwa kuanzia unatekelezwa katika Wilaya ya Ilemela na Nyamagana, ambapo unatarajia kufikia walengwa 125,000. 

Alisema mradi huo unaendelea kutekelezwa katika Wilaya hizo na wameshafanya  mafunzo kwa wahudumu wa afya 198 na viongozi wa kijamii 95 kutoka katika maeneo mbalimbali ya Kata  kwa ajili ya kusaidia kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu na njia bora za udhibiti wa taka ngumu na taka vinyesi katika ngazi za Kaya, kutumia njia sahihi za kupakua vyoo pindi vinapojaa,utenganishaji wa taka ngumu hadi sasa takribani wananchi 90,007 wamefikiwa na elimu hiyo.

"Pia mradi kwa kushirikiana na uongozi wa Kata na Mitaa husika umefanikisha kutambua vikundi vinavyojihusisha na ujasiliamali wa usafi wa mazingira, navyo pia vilipatiwa mafunzo ya ujasiliamali wa usafi wa mazingira na hivi leo tunawapatia vitendea kazi (bajaji) ili waweze kutoa huduma za kuzoa na kusafirisha taka hadi kwenye vituo vya kuchakata taka"alisema James.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza,Mkuu wa Idara ya Usafi  na Mazingira wa  Halmashauri hiyo Danford Kamunya, amesema Jiji la Mwanza linazalisha kwa siku wastani wa tani 250 za taka ambapo  kwa mazingira ya mji ulivyo  wanafikia asilimia 50.

Alisema bajaji hizo zitakua chachu ya kuongeza kipato hali itakayosaidia kuimarisha vikundi hivyo  na jamii ya kata ya Mkuyuni na Buhongwa.

"Siku ya leo tumeweza kupokea pikipiki ya magurudumu matatu (bajaji) mbili kwa ajili ya kusaidia ukusanyaji wa taka taka hapa kwenye maeneo ya Jiji la Mwanza,zitasaidia kupanua wigo wa uzoaji taka katika Kata ya Mkuyuni na Buhongwa kwani mazingira ndio kila kitu ukiyaharibu ni hatari kwa afya ya Jamii,tunaamini mazingira yakiwa safi jamii itakuwa na afya njema ambayo itasaidia kufanya shughuli zao za kiuchumi na kuleta maendeleo ya taifa,"amesema Kamunya

Sanjari na hayo aliwataka watendaji wa kata husika  wasimamie bajaji hizo na zifanye kazi iliyokusudiwa na watafute dereva mwenye leseni atakayeendesha bajaji hiyo.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya  Manispaa ya  Ilemela John Wanga, amelishukuru shirika hilo kwa kuguswa kushirikiana na Serikali kupitia Halmashauri hiyo ya Ilemela kwa suala la uondoaji taka katika maeneo ya Manispaa hiyo.

"Halmashauri ndio mhusika mkuu wa kuhakikisha wananchi  wanaishi katika maeneo safi,kwani wakiwa na afya njema itasaidia kuchochea uchumi na  maendeleo ya taifa,pia aliwapongeza kwa kusema wameenda mbali kwa kuanzisha na kujenga kituo cha mafunzo  ya kutengeneza mkaa kupitia taka taka,kwani litasaidia kuokoa miti na kuweka mazingira safi na salama,huku  elimu watakayo ipata itasaidia wananchi  kutumia majiko au mkaa bila ya kukata miti," amesema Wanga.

Kwa upande wake Ofisa Usafishaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Daniel Paul,amesema Halmashauri hiyo kwa siku inazalisha  tani 479  za taka na wanafikia asilimia 73 huku na tani zinazibaki zipo kwenye maeneo kama ya  vijijini.

Habari Kubwa