Anayedaiwa kubaka mtoto asomewa mashtaka matano

25Mar 2020
Pendo Thomas
Kigoma
Nipashe
Anayedaiwa kubaka mtoto asomewa mashtaka matano

MAHAKAMA ya Wilaya ya Kigoma, imeanza kumsomea maelezo ya awali mshtakiwa Jeremia Kirahunja (49), anayekabiliwa na makosa matano ya kubaka mtoto wa miaka sita kwa miaka mitano mfululizo.

Mshtakiwa huyo anakabiliwa na makosa matano ya ubakaji kesi namba 19 ya mwaka 2020 kosa alilolitenda kwa nyakati tofauti na maeneo tofauti dhidi ya mtoto huyo.

Akisoma maelezo ya awali ya makosa hayo, Wakili wa Serikali, Reymond Kimbe, mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Kitalo Mwakitalu, alisema mshtakiwa alitekeleza makosa hayo katika eneo la Airport mara mbili na Katubuka mara tatu, tangu mtoto huyo akiwa darasa la kwanza hadi darasa la tano alipofikisha miaka 10 baada ya mzazi wake kubaini.

Wakili Kimbe alisema kosa hilo ni kinyume na kifungu cha 130 kifungu kidogo cha kwanza na cha pili (e) na kifungu cha 131 kifungu kidogo cha tatu cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2002.

Mshtakiwa aliposomewa makosa yake, alikana na kesi hiyo imepangwa kusikilizwa tena Aprili 9.

Habari Kubwa