Anayedaiwa kujinyonga aliandika wosia mzito

01Aug 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Anayedaiwa kujinyonga aliandika wosia mzito

MKURUGENZI Msaidizi wa Miradi inayotekelezwa na Umoja wa Ulaya (EU) kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, Leopold Lwajabe (56), aliyekutwa amejinyonga mkoani Pwani, aliacha wosia ofisini kwake, imebainika.

Marehemu Wizara ya Fedha na Mipango, Leopold Lwajabe.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa,  aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Jumatatu ya wiki hii, wafanyakazi wenzake waligundua kuwa Lwajabe aliacha ‘notebook’ kwenye meza yake ofisini ikiwa na ujumbe  wa mgawanyo wa mali zake.

"Lwajabe ambaye ni mkazi wa Kinyerezi, aliacha ‘notebook’ juu ya meza ofisi kwake ikiwa na ujumbe wa mgawanyo wa mali zake kwa familia yake na kwenye msiba wake ametaka wachinjwe ng'ombe wanne," alisema.

Kamanda Mambosasa alisema Julai 26,  saa 2:00 asubuhi, zilipokewa taarifa kutoka kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Mgoza, Kiparang'anda wilaya ya Mkuranga, Mohamed Said (68) kuwa kuna mwili umeonekana kijijini hapo.

"Mwenyekiti huyo aliarifu kuwa kuna mwili wa mwanamume ukiwa umening'inia kwenye mti wa mwembe. Polisi walifika eneo la tukio na kuukuta. Uchunguzi wa awali ulibaini kuwa eneo la tukio hapakuwa na viashiria vyovyote vya kujitetea wakati wa tukio.

"Mwili haukuwa na jeraha lolote isipokuwa shingoni kulikuwa na kamba ya nailoni aliyotumia kujinyonga. Mwili wake ulishushwa na kufanyiwa upekuzi na kwenye mfuko wa kulia wa suruali zilikutwa Sh. 90,000 na mfuko wa kushoto Sh. 98,000 na saa ya mkononi," alisema Mambosasa.

Kamanda Mambosasa alisema mfuko wa nyuma kulikuwa na pochi ndani yake iliyokutwa Dola 10 za Marekani na kitambulisho cha mpigakura.

"Wananchi waliitwa kuutambua mwili huo lakini hakuna aliyemfahamu. Baada ya hapo, mwili ulichukuliwa na kuhifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga kwa utambuzi na uchunguzi wa daktari na kufungua jalada la kosa la kujinyonga," alisema.

Mambosasa alisema upelelezi uliendelea ikiwa ni pamoja na kuwatafuta ndugu wa marehemu.

Alisema Jumatatu ya wiki hii saa 5:00 asubuhi, walipatikana ndugu, Meneja Beichumira ambaye ni mwalimu mkazi wa Babati, mkoani Manyara na mfanyakazi mwenzake, Jonathan Herman.

"Wote kwa pamoja waliutambua mwili na kueleza kuwa Julai 25, saa 12:00 asubuhi, Lwajabe alitoka nyumbani kwake kwenda ofisini akiwa na dereva wake na baadaye alimtuma dereva amfuatie simu yake aliyokuwa ameisahau nyumbani kwake Kinyerezi,” alisema na kuongeza kuwa simu hiyo ilibainika ilikuwa imefutwa kila kitu.

Alisema baada ya dereva huyo kuondoka kwenda Kinyerezi, Lwajabe alitoweka ofisini na kwenda kusikojulikana hadi Julai 26, alipogundulika akiwa amejinyonga huko Mkuranga.

"Hata hivyo, taarifa kutoka kwa mfanyakazi mwenzake zinasema kuwa Lwajabe  alikuwa amepunguza kasi katika utendaji jambo ambalo si kawaida yake na hata kazi za muhimu alikuwa akimpa msaidizi wake azifanye," alisema.

Kwa mujibu wa Mambosasa, mwili wake umehamishiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa uchunguzi zaidi. Alisema  licha ya kifo chake kusababishwa na kujinyonga, chanzo hicho bado kinachunguzwa.

Habari Kubwa