Anayewatuhumu polisi adai hana uwezo kwenda Mwanza

17Jun 2019
Romana Mallya
DAR
Nipashe
Anayewatuhumu polisi adai hana uwezo kwenda Mwanza

SIKU tatu baada ya Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kumtaka mkazi wa jijini Dar es Salaam, Nixon Moshi, aende mkoani humo baada ya kuwatuhumu askari watatu kumpora Sh. 1,188,000, amedai mwongozo wa nani atakaye gharamia nauli na malazi yake.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Jumanne Muliro.

Moshi aliliambia Nipashe jana kuwa yupo tayari kwenda Mwanza kuitikia wito huo wa Jeshi la Polisi, lakini kwa sasa hana nauli wala fedha za kujikimu atakapokuwa mkoani humo.

Ijumaa iliyopita, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Jumanne Muliro, alimtaka Moshi kwenda mkoani Mwanza kwa sababu jalada la kesi ndiko lililofunguliwa.

Akizungumzia wito huo wa kamanda, Moshi alisema yupo tayari kwenda ingawa kwa sasa hana fedha.

"Nipo tayari kwenda Mwanza, lakini kwa sasa sina fedha ya nauli na ya kujikimu wakati wote nitakaokuwa Mwanza, ninaomba Jeshi la Polisi linisaidie mwongozo kwa sababu linashikilia fedha zangu, je, litanisaidia kuniwezesha kufika Mwanza na fedha za kujikimu," alihoji.

Hata hivyo, Moshi alisema mwishoni mwa wiki iliyopita alipeleka barua ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) na kupokelewa na msaidizi wake ambaye alimpa wiki moja ndipo awasiliane naye kujua nini hatima ya fedha zake.

Aidha, Moshi aliandika barua ya wazi kwa IGP, Simon Sirro, akiomba ichapishwe gazetini ili aweze kumsaidia arudishiwe fedha zake anazodai walichukua askari hao.

Alipotafutwa Kamanda Muliro kuhusu madai hayo, alimtaka Moshi aende Mwanza kwa sababu

jalada la kesi limefunguliwa mkoani humo na kwamba tayari Mkuu wa Upelelezi Mkoa Mwanza (RCO) ameshapewa maelekezo.

Habari Kubwa