Angalizo TCRA usajili laini za simu

06Dec 2017
Nebart Msokwa
Nipashe
Angalizo TCRA usajili laini za simu

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imewaonya wananchi wanaotoa vitambulisho vyao kwa watu wengine kwa ajili ya kusajilia laini za simu na kuwataka kuacha mara moja tabia hiyo kwa vile wanaweza kujikuta matatani endapo laini hizo zitatumika kwenye matukio ya uhalifu.

Onyo hilo lilitolewa jijini Mbeya na Ofisa wa watumiaji wa huduma na bidhaa za mawasiliano, Walter Maliki, wakati wa mafunzo maalum kwa waandishi wa habari kuhusu utaratibu mpya wa kusajili laini za simu.

Maliki alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano  na Posta ya 2010,  kila Mtanzania anayetumia simu anatakiwa kusajili laini yake kwa kutoa taarifa sahihi kwa watoa huduma.

Alisema awali wakati zoezi linaanza 2009, watu walikuwa wanaruhusiwa kutumia mpaka barua ya ofisa mtendaji, kitambulisho cha kazi na kitambulisho cha chuo, lakini utaratibu umebadilika na vitambulisho hivyo havitumiki.

Alisema vitambulisho vinavyohitajika ni kitambulisho cha Taifa, kitambulisho cha Mzanzibari mkazi, kitambulisho cha mpigakura, hati ya kusafiria na leseni ya udereva.

“Mtu mwingine akitumia kitambulisho chako kusajili laini, ile laini inakuwa na taarifa zako, kwa hiyo ikitokea mtu huyo akaitumia laini hiyo kwenye tukio lolote la uhalifu, wewe ndiye unawajibika kisheria, hivyo wananchi wajiepushe kufanya hivyo,” alisema Maliki.

Hata hivyo alisema ikibainika mtu alitoa taarifa za uongo wakati wa kusajili laini ya simu yake, faini ni Sh. 3000,000 au kifungo cha miezi 12 jela ama vyote viwili, na kwamba kwa mtu kutumia laini ambayo haijasajiliwa faini yake ni Sh. 500,000 au kifungo cha miezi mitatu jela.

Meneja wa TCRA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Lilian Mwangoka, alisema mtu pekee anayestahili kusaidiwa katika usajili wa laini kwa kutumia kitambulisho ambacho sio cha kwake ni mtoto ambaye hajafikisha umri wa miaka 18.

Alisema hao wanastahili kusaidiwa na wazazi wao kusajili, lakini akatahadharisha kuwa lazima mzazi ajiridhishe na tabia za mtoto wake.