Anusurika kifo kwenye uzazi

15Jun 2019
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Anusurika kifo kwenye uzazi

MKAZI wa Kijiji cha Marasibora, Wilaya ya Rorya mkoani Mara, Belinda Nashon (19), amenusurika kifo baada ya kukosa gari la wagonjwa la kumpeleka kituo cha afya kujifungua na kusababisha kujifungulia zahanati, hali iliyomfanya kutoka damu nyingi na kupoteza fahamu.

mkunga akimfanyia vipimo mama mjamzito.picha na mitandao

Ofisa Muuguzi Mkunga wa Zahanati ya Nyanchabakenye wilayani hapa, Nangi Jacob, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo baada ya Belinda kufika katika zahanati hiyo akiwa katika hali ya kuumwa uchungu.

Jacob alisema ilipofika saa 3:30 usiku, hali ilibadilika baada ya Belinda kujisikia kusukuma mtoto na alimsaidia kwa kuzingatia taaluma yake ya uuguzi na mama huyo alifanikiwa kujifungua mtoto wa kiume ambaye alikuwa na afya njema.

"Baada ya kujifungua huyu mama alipatwa na shida ya kutoka damu nyingi sana na kama unavyojua hii ni zahanati na usiku ule nilikuwa peke yangu ilibidi kuomba msaada kwa ndugu wa mama huyo ambaye alichukua simu yangu na kupiga simu Kituo cha Afya Utegi ili walete ambulance (gari la wagonjwa) ambapo nilijibiwa kuwa gari halina mafuta," alisema Nangi.

Alisema akiwa amevaa gloves aliendelea kumwambia ndugu wa Belinda kutafuta jina la mratibu wa afya ya uzazi na mtoto wa wilaya hiyo, ambaye alifanya jitihada za kutafuta mafuta na kwenda haraka zahanati hapo na kumchukua mzazi huyo aliyekuwa ameshapoteza fahamu na kumfikisha kwenye hospitali kubwa ya misheni ili kuokoa maisha ya Belinda.

Kwa upande wake Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto wilayani hapa, Neema Mwijarubi, alisema siku hiyo kulikuwa na sherehe ya wauguzi Musoma mjini, lakini yeye hakujisikia kwenda alikuwa amelala nyumbani kwake na kushtushwa na simu muda wa saa tano usiku kuwa kuna mzazi amezidiwa na gari la wagonjwa halina mafuta.

"Kweli gari lilikuwa halina mafuta ila tulijitahidi tukaweka, lengo tuweze kuokoa maisha ya huyu mama, maana baada ya kufika pale niliona damu imejaa ndoo nikamuuliza yule muuguzi kama aliongeza maji akasema hapana zilikuwa damu na niligundua alikuwa amechanika, pia damu ilikua ni Hb 3 ambayo ni kiwango kidogo sana," alisema Mwijarubi.

 

Alisema wakiwa njiani kumkimbiza huyo mzazi hospitali kubwa ya misheni Kowaki, Belinda alikuwa amepoteza fahamu, huku upumuaji ukiwa chini hali iliyomfanya aagize waandae mashine ya oxygen na walipomfikisha akiwa na dripu mbili za maji baadaye walimuongeza damu dripu tatu na saa tisa usiku Belinda alirejewa na fahamu zake kama kawaida  na siku iliyofuata aliruhusiwa kurudi nyumbani.

Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo, Blacius Mganyizi, alisema zahanati hiyo inakabiliwa na upungufu wa watumishi ikiwa na wafanyakazi sita pekee.

Aliiomba serikali kuongeza majengo kwa kuwa kwa sasa kuna chumba kimoja cha wajawazito kujifungulia.

Kufuatia tukio hilo Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adamu Malima, alitoa zawadi ya Sh. milioni moja kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya afya kuitoa kwa wauguzi wote waliopambana kuokoa uhai wa Belinda  na mtoto wake."Kwa mujibu wa takwimu za Tanzania Demographic Health Survey (TDHS) ya mwaka 2015/16 katika mkoa wa Mara, wajawazito waliojifungulia kituoni ilikuwa ni asilimia 50 chini ya kiwango cha taifa ambacho ni asilimia 63,  wazazi waliosaidiwa na watoa huduma wenye ujuzi walikuwa ni asilimia 51 chini ya kiwango cha taifa ambacho ni asilimia 64,”  alisema.

Habari Kubwa