Anusurika kifungo rushwa ya 5,000/-

06Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
Morogoro
Nipashe
Anusurika kifungo rushwa ya 5,000/-

DEREVA wa gari aina ya Toyota Noah linalofanya safari kati ya Mikumi na Ifakara mkoani Morogoro, Rashid Katunda, amenusurika kifungo cha mwaka mmoja jela baada ya kupatikana na hatia ya kumhonga askari wa usalama barabarani Sh. 5,000.

Katunda amenusurika kwenda jela baada ya kulipa Sh. 300,000 aliyotakiwa kulipa au kutumikia kifungo hicho.

Hukumu hiyo ilitolewa juzi na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kilombero, Luzango Khamsin baada ya kumtia hatiani mshtakiwa kwa kosa hilo.

Kwa mujibu wa mashitaka, Katunda ambaye hufanya safari zake katika barabara kati ya Mikumi na Ifakara, alimhonga Koplo Elvis aliyekuwa akitekeleza majukumu yake katika barabara ya Ifakara - Morogoro ili asichukuliwe hatua za kisheria.

Mshtakiwa alikuwa akikabiliwa na makosa ya usalama barabarani ya kutokuwa na leseni ya udereva na uchakavu wa bodi ya gari.

Kwa mujibu wa taarifa ya Takukuru, Katunda alikamatwa na maafisa wa taasisi hiyo Januari 29, mwaka huu na kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kilombero ambapo alifunguliwa kesi ya jinai.

Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Ainainyi Minja, aliielezea mahakama kuwa Katunda alishtakiwa kwa kosa la kutoa hongo kinyume na kifungu cha 15 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007.

Baada ya upande wa mashtaka kutoa ushahidi pasi na shaka, Mwendesha Mashtaka aliiomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa mshtakiwa na wengine wanaotenda makosa kama hayo.

Akitoa hukumu hiyo, Khamsin alisema anamhukumu adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa faini baada ya kuridhika na ushahidi uliowasilishwa mahakamani na Takukuru.

Hata hivyo mshtakiwa alitekeleza adhabu ya kulipa faini ya Sh.300, 000 juzi.

Habari Kubwa