Apata msaada baada ya taarifa kuchapishwa Nipashe

19Apr 2022
Christina Mwakangale
DAR ES SALAAM
Nipashe
Apata msaada baada ya taarifa kuchapishwa Nipashe

ASASI ya Mama Africa Foundation (SAMAFO) na wadau wa elimu, wamelishukuru gazeti la Nipashe kwa kutoa taarifa kuhusu Mwanafunzi Bahati Ngolikwa (14), na kuwezesha kupata msaada wa kuchangiwa fedha ili kujiunga na kidato cha kwanza.

Mwanafunzi Bahati Ngolikwa.

Bahati ambaye alihitimu darasa la saba Shule ya Msingi Juhudi, iliyopo Halmashauri ya Mbeya Vijijini, mwaka, mwaka jana, alichaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Vipaji ya Wasichana Galijembe, mwaka huu, ingawa alishindwa kujiunga kutokana na vikwazo mbalimbali.

Wiki iliyopita Gazeti la Nipashe lilichapisha taarifa gazetini kuhusu Bahati, akiomba msaada kielimu kutoka kwa wadau kutokana na mama na baba yake kumtelekeza na kupelekea kuishi na bibi na babu yake, ambao hawana uwezo kifedha.

Mkurugenzi Mtendaji wa Sauti ya SAMAFO, Tabitha Bugali, akizungumza na gazeti hili leo, amesema anatoa shukrani baada ya kufanikiwa kumfikisha shuleni binti huyo baada ya kupatikana fedha za awali kutoka kwa wadau.

Amesema kati ya fedha zinazohitajika takribani Sh. 980,000 zimepatikana Sh. 436,000 ambazo zimemfanya binti huyo kuripoti shuleni ili kuanza masomo kwa muhula wa kwanza.

“Mungu awabariki gazeti la Nipashe na wadau wote ambao wengi hakutaka kutaja majina yao. Bahati ameripoti shuleni mwishoni mwa wiki,” amesema Tabitha.

Aidha, amesema kwa wale ambao wataendelea kuguswa watumie akaunti ya shule hiyo kumchangia binti huyo, ambayo ni Galijembe Girls Secondary School - NMB A/C Namba 61010036195.

Akizungumza awali Bahati amesema ana ndoto ya kuwa daktari. Amesema kuwa kwa sasa anaishi  kitongoji cha Iwindi, kata ya Iwindi, pamoja na bibi na babu yake na wadogo zake wawili ambao hawamjui baba yao huku mama yao mzazi akiwatelekeza miaka mingi.

“Nilijisikia furaha kubwa nilipochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka wa masomo 2022, changamoto ilikuwa malipo ya ada nilikochaguliwa, lakini Sasa nipo shuleni ninashukuru,” amesema Bahati.

Habari Kubwa