Apongeza shirika kuokoa mabilioni

18Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
 MISENYI
Nipashe
Apongeza shirika kuokoa mabilioni

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula, amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kwa kuokoa mabilioni ya shilingi yaliyokuwa yatumike kujenga Kitega Uchumi cha Mtukula kilichoko Misenyi mkoani Kagera.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akisaini kitabu cha wageni kupitia mgongo wa Katibu wake Elias Ndalichako alipokwenda kukagua ujenzi wa jengo la kitega uchumi la Shirika la Nyumba la Taifa lilipo Mtukula wilaya ya Misenyi mkoa wa Kagera akiwa katika ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi mwishoni mwa wiki. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Misenyi Kanali Denis Mwila.

Mabula alitembelea mradi wa ujenzi wa jengo hilo wakati akiwa kwenye ziara ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia sekta ya ardhi katika Wilaya ya Misenyi mwishoni mwa wiki.

Alieleza kufurahishwa na gharama ndogo zilizotumika katika ujenzi wa kitega uchumi hicho cha NHC Mtukula baada ya kuelezwa na Mhandisi wa Ujenzi, George Shanel, kuwa hadi sasa, gharama yake imefikia Sh. milioni 800 wakati jengo limefikia asilimia 80 ya ujenzi.

Kiwango hicho ni tofauti na makadirio yaliyoelezwa awali kuwa lingegharimu Sh. bilioni tatu kama ujenzi huo ungefanywa na kampuni ambayo ingepewa zabuni.

Mabula alilipongeza shirika kwa kuokoa fedha nyingi kwa kutumia kampuni yake ya ujenzi na kutoa wito kwa taasisi mbalimbali nchini kulitumia shirika hilo kujenga ofisi na nyumba za watumishi kwa kuwa lina uwezo mkubwa katika ujenzi.

Jengo la kitega uchumi la NHC Mtukula liko mpakani mwa Tanzania na Uganda, litakapokamilika, litakuwa na ofisi mbalimbali zikiwamo za benki na maduka 36.

Mabula alisema kufanya vizuri kwa shirika hilo kumejionyesha katika kazi za ujenzi wa ofisi za wizara mbalimbali katika Mji wa Serikali Ihumwa mkoani Dodoma, linakojenga ofisi za wizara mbalimbali zikiwamo Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Fedha na Mipango.

Alidai ujenzi unaotekelezwa na shirika hilo Ihumwa unakwenda kwa haraka na ubora wa uhakika.

Habari Kubwa