Arusha sasa yaahidi kutengeneza mazingira mazuri kwa wawekezaji

02Mar 2016
John Ngunge
Arusha
Nipashe
Arusha sasa yaahidi kutengeneza mazingira mazuri kwa wawekezaji

SERIKALI mkoani humu, imeahidi kuwa itaendelea kutengeneza mazingira mazuri kuvutia wawekezaji katika nyanja mbalimbali.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha ,Felix Ntibenda.

Akizungumza katika uzinduzi wa kituo cha kuuza mafuta cha Total kilichopo Makuyuni wilayani Monduli jana, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Francis Miti, alisema serikali itaendelea
kutoa ushiriakiano wa kutosha kuhakikisha wawekezaji wanavutiwa na kuendelea kuwekeza katika maeneo mbalimbali.

Alisema sera ya nchi ni kuwapokea wawekezaji na kulinda mitaji, kazi zao na kuhakikisha wanafanya bila kubughudhiwa na mtu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanashirikiana vyema na jamii inayowazunguka kwa kufuata sheria na taratibu ili kuvutia wawekezaji wengine.

Aidha, alisema uwapo wa kituo hicho utatoa huduma kwa wananchi wengi wakiwamo madereva wa magari ya utalii wanaofanya shughuli zao katika Hifadhi za Taifa kama vile Manyara na Tarangire, Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

“Sisi tunashukuru kampuni hii kuja kuwekeza katika eneo hili ambalo ni njia panda na bidhaa hii ilikuwa tabu sana kuipata katika maeneo haya hivyo basi wametoa ajira na kuahidi kuendelea kutoa kwa akina mama katika mgahawa wake hivyo basi ni fursa na nina hakika wananchi watanufaika na kituo hiki,’’ alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Total Tanzania,Tarik Moufaddal, alisema kampuni hiyo imejipanga kutoa huduma bora ikiwepo mafuta bora na kuhudumia wananchi kwa kuchangia maendeleo yao ikiwamo kutoa misaada mbalimbali katika sekta ya elimu kwa kutoa madawati na
kuboresha miundo mbinu.

Pia alisema kituo hicho mpaka sasa kimetoa ajira za kudumu na za muda kwa watu 15 hivyo kuisadia serikali kupambana na tatizo sugu la ajira, ikiwa ni pamoja na kuwauzia wananchi vifaa vya umeme wa jua kwa bei nafuu ili kuwawezesha wananchi kukabiliana na changamoto ya kukosa
nuru yaani mwanga.

Nao baadhi ya waendesha bodaboda akiwapo Humphrey Zephania, pamoja na Samwel Mollel, walisama ujio wa kituo hicho kutawawezesha kupata huduma ya mafuta saa 24 kwa kuwa hapo awali walikuwa wanafuata mafuta katika
eneo la Mto wa Mbu, Karatu na wakati mwingine Arusha mjini kutokana na kukosa kabisa kituo cha mafuta katika wilaya hiyo.

''Muda mwingine pindi ambapo kunakuwepo na tatizo la umeme tunakosa kabisa huduma ya mafuta lakini sasa muda mwingi hapa pako wazi hivyo kutuwezesha kufanya shughuli zetu masaa ishirini na manne bila kujali umeme upo ama haupo," alisema.

Pia aliiomba serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini kuthibiti ubora wa mafuta na wakati mwingine kuzuia upandishaji wa bei ya mafuta kiholela kwa kuwa unawaathiri katika utendaji kazi wao ikiwapo kuvifungia kabisa vituo hivyo.

Habari Kubwa