ASA yakabidhiwa jukumu kuzalisha mbegu bora

10Aug 2020
Christina Haule
Morogoro
Nipashe
ASA yakabidhiwa jukumu kuzalisha mbegu bora

​​​​​​​WAKALA wa mbegu Tanzania (ASA) imejipanga kuzalisha mbegu bora za pamba kufuatia kukabidhiwa jukumu la kuzalisha mbegu bora za zao hilo katika hekta 11.1 zilizopo Igunga mkoani Tabora ili kuongeza uzalishaji na kufikia lengo la Serikali la kuanzia kiwanda cha uchakataji wa mbegu mkoani-

Afisa Kilimo Msaidizi, Juma Wilson, akionesha kitalu cha mbegu za pamba aina ya UKM 08 katika viwanja vya maonesho ya kilimo 88 Kanda ya Mashariki.

-humo ili kuwapatia wakulima mbegu bora.

Kaimu Meneja Uzalishaji wa mbegu kutoa ASA, Benjamin Mfupe, amesema hayo jana kwenye maonesho ya wakulima 88 Kanda ya mMashariki yaliyofanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere yanayohusisha mikoa ya Morogoro, Pwani, Tanga na Dar es salaam ambapo amesema Serikali imeamua kukabidhi jukumu hilo kwa ASA kwa sababu wao ndio wanaoshughulika na upatikanaji wa mbegu bora nchini.

Amesema kwa kukabidhiwa hekta hizo 11.1 ambazo ni sawa na vijiji 60 watasaidia namna ya kupata mbegu bora na hivyo kuhakikisha uzalishaji wa mbegu hizo unaongezeka huku wakulima wakizipata kwa wakati.

Mfupe amesema kwa kutumia mbegu aina ya UKM 08 watahakikisha wanawasimamia wakulima kutokana na mashamba hayo kulimwa na wakulima na kusimamiwa na ASA na kuhakikisha wanafuata kanuni za kilimo ili kupatikana mbegu bora kwa ajili ya kilimo bora.

“kwa kushirikiana na vyama vya ushirika vya msingi AMCOS na watafiti wa kilimo tutahakikisha tunapata mbegu bora hata pamba ikifikishwa katika hatua za kwanza kwenye kiwanda kikifunguliwa” amesema Mfupe.

Awali Afisa kilimo msaidizi Juma Wilson amesema katika msimu wa mwaka 2021 katika uzalishaji mbegu za zao hilo watashirikiana na wakulima wa mkataba ili kuweza kuongeza uzalishaji zaidi.

Amesema mbegu hiyo UKM 08 ambayo imethibitika kufanya vizuri katika uzalishaji wake na mkulima kupata tani 20 za pamba kwa hekari moja wakati kwa mbegu zingine mkulima hupata tani 10 ambapo mbegu hiyo itamfikia mkulima katika msimu ujao wa kilimo kuweza kupiga hatua kwenye kilimo hicho cha zao la biashara.

Wilson amesema uzalishaji wa mbegu bora za zao la Pamba utasaidia kukuza mnyororo wa thamani kwa mkulima kwa sababu mkulima anazalisha Pamba anapeleka kiwandani inatengenezwa nguo kisha nguo inarudi tena kwa matumizi ya mavazi kwa mkulima.

Hata hivyo amewashauri wakulima kutoka mikoa inayolima Pamba kwa wingi ikiwemo Tabora, Mwanza, Shinyanga, Mara, Katavi na mikoa mingine nchini kuanza kufanya mawasiliano na ASA kwa ajili ya kupata mbegu bora za Pamba katika msimu ujao wa kilimo.

Habari Kubwa