Asakwa na polisi kwa tuhuma ya kuhifadhi wahamiaji haramu

02Mar 2016
Margaret Malisa
Pwani
Nipashe
Asakwa na polisi kwa tuhuma ya kuhifadhi wahamiaji haramu

JESHI la Polisi Mkoani Pwani linamsaka mkazi wa Kilangalangala Mlandizi, wilayani Kibaha, kwa tuhuma za kuwahifadhi raia 35 wa Ethiopia kinyume cha sheria.

Wahamiaji haramu.

Wahamiaji hao haramu walibainika baada ya majirani wa kijana huyo kutoa taarifa polisi kuwa wana wasiwasi nae kutokana na mara kadhaa kuonekana akirudi usiku na magari makubwa huku akiteremsha makundi ya watu ambao hawaonekani mchana.

Akizungumza mjini hapa jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Bonivetura Mushongi, alisema raia hao wa Ethiopia walikamatwa juzi, saa 5.30 usiku, nyumbani kwa mtuhumiwa huyo aliyebainika kuwa ni kinara wa kuwahifadhi na kuwasafirisha wahamiaji haramu kutoka Ethiopia na Sudan.

Alisema polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema na kwenda kupekuwa nyumba hiyo na kuwakamata wahamiaji hao ambao hawakuwa na vibali vya kuwaruhusu kuishi nchini na kwamba aliyekuwa akiwahifadhi alikimbia na kuwatelekeza kwa kuhofia kukamatwa.

Kamanda Mushongi alisema wahamiaji hao haramu waliingia nchini wakitokea Mombasa nchini Kenya kupitia mkoa wa Tanga kwa njia ya barabara kwa kutumia usafiri wa Fuso na Noah na kufikia katika nyumba hiyo wakijiandaa kwa safari ya kwenda Afrika ya Kusini.

Alisema watuhumiwa wote watakabidhiwa kwa Idara ya Uhamiaji Mkoa wa Pwani kwa kwa ajili ya hatua zaidi ikiwamo za kisheria.

Habari Kubwa