Asasi za kiraia zatakiwa kufanya kazi kwa tija

30Jul 2021
Christina Mwakangale
DAR ES SALAAM
Nipashe
Asasi za kiraia zatakiwa kufanya kazi kwa tija

WITO umetolewa kwa asasi za kiraia kufanya kazi kwa tija na kufuata sheria, wajibu na weledi ili kuletea maendeleo kwenye jamii ambayo, inahitaji huduma mbalimbali ikiwamo za kiafya, kielimu na kiuchumi.

Mwenyekiti wa Baraza la Uratibu wa NGOs Taifa (NaCoNGO), Lilian Badi.

Mwenyekiti wa Baraza la Uratibu wa NGOs Taifa (NaCoNGO), Lilian Badi ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam kwenye uzinduzi wa wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI), ulioshirikisha asasi tofauti nchini.

Amesema asasi hizo ni muhimu kukutana ili kujifunza na kubadilishana uzoefu na kwamba NaCoNGO itaendelea kushirikiana nazo hususan katika kufanya maboresho na mageuzi kwa mujibu wa sheria.

“Ni muhimu kutambua kwamba taasisi ya Foundation for Civil Society (FCS), imekuwa kinara katika kuzijengea uwezo AZAKI, kupitia ruzuku hata mafunzo mblaimbali. Tunapozindua wiki ya AZAKI ni ushahidi ufanisi na dhamira ya asasi kufikia mafanikio,” amesema Lilian.

Aidha, Lilian amesema FCS pamoja na wadau wengine kuendelea kuunga mkono NaCoNGO na kutekeleza majukumu yao kisheria, na kwamba hatua hiyo itasaidia kupungua kwa migaogoro ya mara kwa mara isiyo na toja kwenye asasi ambayo hudhoofisha utendaji.

Mkurugenzi Mkuu wa FCS, Francis Kiwanga amesema katika kuanndaa wiki ya AZAKI itakayoanza Oktoba 25 hadi 29, mwaka huu wanatarajia kumualika Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni rasmi na kwamba lengo ni kutathmini kazi zao na kuongeza maeneo ya kimkakati.

“Ili kuleta tija katika maeneleo nchini ni kazi ya serikali lakini serikali haiwezi pekee, inatakiwa kila mmoja kuchangia, AZAKI tunatakiwa kutoa mchango wetu na nguvu kuelekeza nguvu zetu zaidi hususan kwenye mpango wa taifa wa miaka mitano,”

Alisema wiki hiyo pia itahusisha maonyesho ili jamii izifahamu AZAKI zilizopo nchini pamoja na majukumu yao kijamii kwa kila asasi ambayo inatambuliwa na serikali.

Mbunge wa Viti Maalumu, Neema Lugangira amesema asasi za kiraia pamoja na NGOs, zikitumia fedha za ruzuku ipasavyo kwenye sekta mbalimbali itasaidia miradi kuwa endelevu

“Mara nyingi asasi za kiraia huwa tunahesabiwa kama sekta binafsi, asasi na NGOs zinasimamaa katika kuchangia maendekeo na si katika kupata faida, ninasema hilo kwa sababu nina taasisi.

“Kuna vijana wanafanya kazi kwangu ambao wanaojitolea nawalipa posho, TRA inawahesabia kama wafanyakazi na kututoza kodi, tunahitaji sheria sahihi,” amesema Neema.

Habari Kubwa