Ashauri walimu wanaofaulisha wanafunzi vizuri watuzwe

21Feb 2017
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Ashauri walimu wanaofaulisha wanafunzi vizuri watuzwe

SERIKALI imeshauriwa kuweka utaratibu wa kuwapa motisha walimu wanaofaulisha vizuri masomo yao kwenye mitihani mbalimbali ya kitaifa.

Hatua hiyo itakuwa ni sehemu ya kutambua michango yao ya kuinua kiwango cha elimu nchini.

Ushauri huo ulitolewa jijini hapa na Ofisa Tawala wa Shule za Kimataifa za St. Mary’s za jijini humu, Anuciata Ngonyani, wakati wa ibada maalumu ya kuombea amani ya nchi, viongozi wa kitaifa, wazazi pamoja na mafanikio ya shule.

Ngonyani alisema motisha humfanya mwalimu aongeze bidii katika ufundishaji kwa kutambua kuwa mchango wake kwenye ufundishaji unatambulika na serikali.

Alisema mbinu hiyo ndiyo inayosaidia shule nyingi za binafsi nchini kufanya vizuri kwenye matokeo ya mitihani mbalimbali ya ushindani hasa ya kitaifa ambayo mara kwa mara shule hizo huongoza.

“Vitabu vitakatifu vinamtaka binadamu kumshukuru Mungu kwa mafanikio yoyote anayoyafikia ili kupata baraka zaidi. Hivyo hivyo hata serikali inatakiwa kuwa na utaratibu wa kutambua michango ya walimu katika kuinua kiwango cha elimu kwa kuwapa motisha,” alisema Ngonyani na kuongeza:

“Shule nyingi za binafsi huwa zifanya hivyo na ndiyo maana miaka yote huonekana bora kuliko za serikali kwenye matokeo ya mitihani mbalimbali. Walimu wanahitaji kutiwa moyo.”

Hata hivyo, alisema katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba mwaka jana, shule yake iliongoza Jiji la Mbeya na kushika nafasi ya pili kimkoa.

Naye Mchungaji wa Kanisa la Rehoboth International Christian Center (RICC) la jijini Mbeya, Sunday Matondo, aliyekuwa mgeni rasmi kwenye maombi hayo, aliwataka wazazi na walezi kuwapa ushirikiano walimu katika ufuatiliaji wa maendeleo ya watoto wao shuleni na kuwarekebisha.

Alisema baadhi ya wazazi hawafuatilii maendeleo ya watoto wao, lakini wanapofeli kwenye mitihani yao ya mwisho, lawama zote huelekezwa kwa walimu na watoto, jambo alilosema siyo sahihi.

Aidha, aliwataka wazazi kuwaombea walimu ambao aliwaita kuwa ni walezi mbadala wa watoto ili wawalee watoto wao katika maadili mema.

Alisema kazi wanayofanya walimu ni ngumu, hivyo wanahitaji kuwa na hekima ili wawalee watoto katika maadili mema kwa muda wanaokuwa nao.

“Walimu wana kazi ngumu ambayo haina mfano, kazi yao inahitaji maarifa na uvumilivu, hivyo wazazi na walezi tunatakiwa kuwaombea na kuwatia moyo ili wawalee watoto wetu katika maadili mema,” alisisitiza Matondo.

“Mara nyingi wanafunzi wakifanya vibaya kwenye mitihani ya kitaifa, mtu wa kwanza kulaumiwa ni mwalimu, kitu ambacho si sahihi sana, hata wazazi wakati mwingine tunatakiwa kulaumiwa kwa sababu hatufuatilii maendeleo yao.

Katola ibada hiyo maalumu, wazazi pamoja na wananchi, walimuombea Rais John Magufuli, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na viongozi mbalimbali wa serikali.

Habari Kubwa