Asilimia 70 Katavi wapatiwa chanjo UVIKO -19

19Jan 2022
Neema Hussein
Katavi
Nipashe
Asilimia 70 Katavi wapatiwa chanjo UVIKO -19

MRATIBU wa chanjo ya kujikinga na ugonjwa wa UVIKO-19 Mkoa wa Katavi, Stephano Kahindi, amewataka wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kupatiwa chanjo hiyo.

Mratibu wa Chanjo ya UVIKO-19 mkoa wa Katavi, Stephano Kahindi, akizungumza na mwandishi wa Nipashe (hayupo pichani) kuhusu hali ya utoaji wa chanjo katika mkoa huo. PICHA: NEEMA HUSSEIN

Akizungumza na Nipashe leo januari 19, 2022 Kahindi amesema, mpaka sasa wananchi 62, 830 wamepatiwa chanjo hiyo sawa na asilimia 70 ya wakazi wa mkoa huo.

Kahindi amesema kuna chanjo aina mbili inayotolewa ambayo ni Sinopharm na Pfizer, huku akisisitiza kuwa chanjo hizo hazina madhara yoyote.

"Mwenendo wa utoaji wa chanjo kwa mkoa wa Katavi tunaendelea vizuri, tuna timu zetu za watalaam wa afya wanaenda kutoa huduma kwa wananchi, tunawafuata wananchi hatuwasubirii kwenye vituo vyetu," amesema.

Kahindi amesema ili mtu apate kinga kamili ya ugonjwa wa korona inatakiwa apate dozi mbili ambapo akipata dozi ya kwanza inatakiwa akae siku 21 ndipo akamilishe dozi ya pili.

Hata hivyo, Kahindi amewatoa hofu wananchi wenye imani potofu kuhusu chanjo ya korona akisistiza ni salama na imethibitishwa na taasisi za ubora ikiwemo WHO, maabara ya mkemia mkuu wa serikali na taasisi zingine.

"Chanjo zipo na kama kuna maswali yoyote waendelee kuwauliza wataalam wa afya sisi tupo tumejipanga na tunatoa huduma saa 24, umuhimu wa chanjo ya korona ni kumkinga mwananchi na madhara ya ugonjwa wa korona na hata akiugua hatopata madhara makubwa ambayo yanaweza kumpelekea kwenye kifo au kulazwa hospitali," amesema.

Amesema kuna baadhi ya wananchi walikuwa hawana elimu juu ya umuhimu wa kupata chanjo hiyo, lakini wao kama wataalam wa afya wameendelea kutoa elimu kwa wananchi na sasa wanaelewa umuhimu wa chanjo hiyo.

Habari Kubwa