Asimulia shuka ilivyomwokoa padri katika ajali ya moto

20Jan 2019
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Asimulia shuka ilivyomwokoa padri katika ajali ya moto

WAKATI mapadri wa Kanisa Katoliki wakipoteza kila kitu kwenye ajali ya moto iliyotokea kwenye makazi yao, Segerea jijini Dar es Salaam, imebainika kuwa mmoja wao alinusurika kifo kwa kutumia shuka.

Padri Thadeus Mattowo wa Jimbo la Musoma mkoani Mara.

Moto huo ulipokuwa unawaka, Padri huyo, Thadeus Mattowo wa Jimbo la Musoma mkoani Mara, imebainika kuwa alikuwa amelala ndani ya jengo hilo lakini mapadri wenzake walimwokoa kutoka kwenye jengo hilo kwa kutumia shuka na kumshusha kutoka juu ghorofani hadi chini akiwa bado amelala.

Mapadri hao ambao wanaishi kwenye nyumba za walimu wa Seminari ya Mtakatifu Karol Lwanga ya Segerea, hawakupata madhara yoyote lakini wamepoteza kila walichokuwa nacho kwenye makazi hayo.

Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu, Askofu Flavin Kasala, alisema jana kuwa mapadri hao, walibakiwa na mavazi waliyo kuwa wamevaa siku hiyo.

Pia alitaja wanachohisi kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme uliokuwa ukipungua na kuongezeka mara kwa mara kabla ya kutokea kwa tukio hilo.

“Tukio lilikuwa hatarishi hata kwa maisha na baadhi ya njia zilizotumika kuwaokoa waliokuwa ndani ya nyumba ni kama hadithi kwa sababu yuko padre aliyeokolewa kwa kutumia shuka,” alisimulia.

Alisema watumishi hao wa Mungu wamepoteza mali zote walizokuwa nazo ndani ya jengo hilo, hivyo wanahitaji msaada wa haraka ili kujikimu.

Kutokana na ajali hiyo, Askofu Kasala alisema wamefungua akaunti kwa ajili ya kupokea michango katika Benki ya Biashara ya Mkombozi na yeyote aliyeguswa na tukio hilo anaombwa kuchangia kwa kutumia namba 00111510990001 yenye jina TEC MAAFA SEGEREA SEMINARY.

Akizungumza na gazeti hili juzi, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Dk. Charles Kitima, alisema chanzo cha moto huo kilikuwa hakijafahamika isipokuwa mapadri wote walisalimika lakini vitu vyao ndivyo vimetetetea.

“Ni nyumba ya makazi ya mapadri walimu. Vyumba 14 vya juu vyote vimeteketea, tunasubiri taarifa kutoka kwa wahusika kujua chanzo cha moto huo na tunashukuru kikosi cha zimamoto kilisaidia kuudhibiti hivyo haukufika kwenye vyumba vya chini,” alisema Dk. Kitima.

Alisema siku mbili kabla ya tukio hilo, kulikuwa na hitilafu ya umeme katika eneo hilo na wahusika walitoa taarifa Shirika la Umeme (Tanesco), ambao walifika na kufanya uchunguzi.

Juzi, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala, Elisa Mugisha, alisema kuwa walipata taarifa za kuzuka kwa moto huo juzi saa 5 usiku na haraka walikwenda kwenye eneo la tukio ili kuzima moto huo.

Alisema walipofika huko walikuta moto umekuwa mkali hivyo waliwasiliana na viongozi wa kikosi hicho Mkoa wa Temeke ili kuongeza nguvu.

Kitima alisema bado moto ulizidi kupamba hivyo waliamua kuwasiliana na kikosi kilichopo uwanja wa ndege ndipo wakafanikiwa kuuzima saa 6.50 usiku huo.

“Taarfa za awali tulizopata ni kwamba moto huo ulianzia kwenye chumba cha Padri Benedict Shemfumbwa, ambaye hakuwa ndani, tunaendelea kukusanya taarifa za uchunguzi ili kubaini chanzo cha moto, ingawa inasadikiwa ni hitilafu ya umeme ,” alisema Kamanda Mugisha.

Habari Kubwa