Askari polisi afia baa akiwa amelewa chakari

15Mar 2019
Gideon Mwakanosya
Songea
Nipashe
Askari polisi afia baa akiwa amelewa chakari

ASKARI  Polisi mkoani Ruvuma,  amekutwa amekufa kwenye baa ya Friend's Pub  iliyoko katikati ya mji wa Songea huku ikielezwa kuwa alikuwa amekunywa pombe kupindukia.

Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma,  Simon Marwa, alimtaja askari polisi aliyekutwa amekufa kuwa ni Konstebo Donald Motoulaya (29), ambaye ni askari katika ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa. Alisema ilidaiwa kuwa siku ya tukio hilo, juzi majira ya saa 4:15 asubuhi, Jaibu Nyoni (26) ambaye ni mhudumu wa baa hiyo, alitoa taarifa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi kuwa askari Donald amelala kwenye kochi na amejaribu kumwamsha lakini imeshindikana. Kamanda Marwa alifafanua zaidi kuwa baadaye askari waliongozana na daktari kwenda eneo la tukio ambako walimkuta askari huyo akiwa amelala kwenye kochi ambalo liko ndani ya baa hiyo. Marwa alisema katika uchunguzi ilibainika kuwa askari huyo alifika kwenye baa hiyo Machi 12, majira ya saa 4:30 usiku akitokea katika baa nyingine iitwayo Mtini Pub ambako alikuwa akinywa pombe. Alisema mtoa taarifa alieleza kwamba wakati askari huyo anaingia Friend's Pub, aliteleza na kuanguka kwenye ngazi na baadaye alimwinua na kumtoa nje kisha askari huyo alirejea na kukaa kwenye kochi wakati huo mhudumu akiendelea kuhudumia wateja. “Ilipofika majira ya saa 4:15 asubuhi jana (juzi), wahudumu wakiwa wanafanya kazi za usafi, ndipo walipomwona PC Donald akiwa kwenye kochi wakidhani amelala lakini walipojaribu kumwamsha hakuamka ndipo walipotoa taarifa polisi. Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Ruvuma, Dk. Hassan Lumbe, alipohojiwa na waandishi wa habari kuhusu  tukio hilo, alisema mwili wa askari huyo ulifikishwa hospitalini hapo na watu ambao hawakujitambulisha na ulipokewa na mganga wa zamu. Dk. Lumbe alifafanua kuwa baada ya kufanya uchunguzi wa kitabibu ilionekana kuwa askari huyo ameshafariki dunia muda mrefu uliopita na kwamba uchunguzi huo ulionyesha hakuwa na mchubuko wowote isipokuwa kulikuwa na mchubuko mdogo kwenye shavu la kushoto.   Alisema baadaye walipohojiwa watu waliomleta walidai kuwa alikuwa amekunywa kiasi kikubwa cha pombe, hivyo uchunguzi wa kitaalam wa sababu ya kifo chake ni kwamba alikuwa amekunywa pombe kwa  kupindukia.