Askari 1,250 wapelekwa DRC kulinda amani

12Apr 2017
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Askari 1,250 wapelekwa DRC kulinda amani

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, amesema tangu mwaka 2013 serikali imepeleka wanajeshi 1,256, katika Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) kwa ajili ya kulinda amani kutokana na migogoro iliyokuwapo katika nchi hiyo.

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi.

Dk. Mwinyi alitoa kauli hiyo jana bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Saleh Ally.

Mbunge huyo alihoji Tanzania imekuwa ikipeleka vikosi vya kulinda amani ndani ya Afrika na sehemu zingine duniani na kwamba masuala kama hayo yanaimarisha jina la Tanzania kwa kiasi gani.

Alihoji kwa miaka 10 iliyopita Tanzania ilipeleka vikosi katika maeneo gani na kwa misingi gani pia ni changamoto gani zinakuwapo katika kukusanya vikosi hivyo kabla havijapelekwa nje ya nchi.

Akijibu maswali hayo, Mbunge huyo alisema Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa na inatimiza wajibu wake wa kuzisaidia nchi zenye migogoro ili kuleta amani ikiombwa kufanya hivyo.

“Ushiriki huu wa Tanzania umewaletea heshima kubwa duniani kwa mara zote kuonyesha utayari wao wa kutoa msaada wa ulinzi na amani,” alisema.

Dk. Mwinyi alibainisha kuwa miaka 10 iliyopita, Tanzania imepeleka vikundi vya ulinzi wa amani Lebanon (kombania mbili tangu mwaka 2008), Darfur Sudan (kikosi kimoja tangu mwaka 2009) na DRC zaidi ya kikosi kimoja cha watu 1,256 tangu mwaka 2013.

Hata hivyo, alisema changamoto wanazozipata katika kukusanya vikundi kabla ya kupelekwa nje ya nchi kwenye majukumu ya ulinzi wa amani ni pamoja na gharama za kuvihudumia vikiwa kwenye mafunzo.

Alitaja changamoto zingine ni vifaa vya wanajeshi vitakavyotumika eneo la uwajibikaji, ugumu wa kupata mafunzo ya uhalisia wa maeneo wanakokwenda kwa mfano jangwani na misituni.

Katika swali la nyongeza, mbunge huyo alihoji serikali ina utaratibu gani pale mwanajeshi anapopoteza maisha au kujeruhiwa akiwa katika nchi nyingine kwa ajili ya kulinda amani.

Ally alisema mara nyingi wanaokwenda kulinda amani katika nchi hizo wamekuwa wakipoteza maisha au kujeruhiwa.

Akijibu swali hilo, Dk. Mwinyi alisema alisema utaratibu wa kuhudumia familia hizo hufanywa na Umoja wa Mataifa (UN) na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuzilipa familia stahiki pindi ndugu yao anapofariki dunia au kupata ulemavu.

Habari Kubwa