Askari FFU alivyojitoa uhai kwa SMG

12Jul 2018
Halima Ikunji
 TABORA
Nipashe
Askari FFU alivyojitoa uhai kwa SMG

ASKARI wa Jeshi la Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Michael Hosea (29), amejiua kwa kujipiga risasi nne shingoni na kutokea utosini na kufariki dunia papo hapo.

Kaimu Kamanda wa Jeshi hilo mkoani hapa, Graifton Mushi.

Akizungumza na Nipashe jana, Kaimu Kamanda wa Jeshi hilo mkoani hapa, Graifton Mushi, alisema tukio hilo lilitokea Julai 10, mwaka huu majira ya saa 11.45 alfajiri.

Graifton alisema, Hosea mwenye namba G.8845 PC alijipiga risasi kwa kutumia silaha aina ya SMG na kufariki dunia.

Kaimu kamanda huyo alifafanua kuwa marehemu alifika ofisi za FFU majira ya saa 11.40 alfajiri na kuanza kusalimia askari wenzake waliokuwa katika eneo hilo na kisha kuingia chumba cha kuchukulia silaha.

Alisema askari huyo alichukua silaha hiyo kwa ajili ya kuingia katika lindo lake kwenye Benki ya Access.

Aidha, alifafanua baada ya kuchukua silaha katika chumba hicho, alitoka kupitia chumba cha walinzi cha kupumzikia kwa ajili ya kwenda foleni ili aingie kazini.

Kamanda alisema kuwa, askari huyo alipofika mlango wa kutoka nje alijipiga risasi nne shingoni ambazo zilitokea utosini na kufariki dunia.

Alisema chanzo cha kujiua askari huyo bado hakijajulikana na uchunguzi unafanyika kuhusu tukio hilo na mwili wa marehemu umesafirishwa kwenda nyumbani kwao Dodoma kwa mazishi.

Omari Bateza askari wa jeshi hilo, alisema wamesikitishwa na tukio hilo, kwa kuwa marehemu  alikuwa ni mchapakazi, mwenye upendo na aliyekuwa akishirikiana na wenzake katika kazi hasa katika lindo lake.

Aliwataka askari wenzake wanapokuwa na matatizo wasichukue uamuzi kama huo bali washirikishe viongozi ili wasaidiwa kimawazo.

 

 

Habari Kubwa