Askari FFU wajitolea damu kusaidia jamii

19Apr 2019
Lilian Lugakingira
BUKOBA
Nipashe
Askari FFU wajitolea damu kusaidia jamii

KATIKA kukabiliana na upungufu wa damu unaoukabili mkoa wa Kagera na kutishia maisha ya makundi yanayoongezeka kuhitaji kuongezewa damu wakiwamo wajawazito wanaojifungua kwa njia ya upasuaji, askari polisi Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wamejitolea kuchangia damu.

Askari hao wamejitolea damu kusaidia makundi hayo wakiwamo watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na majeruhi wa ajali.

 Wakizungumza wakati wa zoezi hilo, baadhi ya askari waliozungumza na waandishi wa habari waliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kujitolea damu, ili kuokoa maisha ya Watanzania wenzao wanaohitaji kuongezewa damu.

Mmoja wa askari hao, Juma Ramadhan, alisema ameguswa na tatizo la watu wanaopoteza maisha kwa sababu ya kukosa damu, na kuwaomba askari wenzake kujitokeza kuchangia damu ili kunusuru maisha ya wananchi wenzao.

Askari mwingine, Slyvester Mazanza, alisema kuwa yeye kama askari anayelinda raia na mali zake hapendi kusikia raia apotee kwa kukosa damu wakati ana uwezo wa kujitolea damu.

“Kuna ndugu zetu kama wajawazito ambao wanapoteza damu nyingi wakati wa kujifungua na watoto, wanahitaji kuongezewa damu, sisi kama askari tumejisikia fahari kushiriki katika zoezi hili,” alisema.

Sajenti Charles Fabian alisema ni vema askari kuwa mfano kuchangia damu na kuwa wao wako tayari kuchangia muda wowote wanapohitajika kufanya hivyo, ili kuhakikisha afya za Watanzania ziko salama.

Kwa upande wake, kiongozi mshauri wa timu ya damu salama mkoa wa Kagera, Amos Bashweka, aliyeongoza zoezi hilo, alisema mkoa unakabiliwa na upungufu wa wastani wa chupa 200 za damu kwa mwezi, kati ya wastani wa chupa 1,000 zinazohitajika.

Bashweka alisema katika zoezi hilo wamefanikiwa kukusanya chupa 50 za damu na kuwa zitawasaidia kukabiliana na upungufu wa damu katika hospitali zao.

Habari Kubwa