Askari polisi waliopiga dereva, abiria mbaroni

19Mar 2019
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Askari polisi waliopiga dereva, abiria mbaroni

JESHI la Polisi linawashikilia askari wake wawili wa Kikosi cha Usalama Barabarani kwa tuhuma za kufanya makosa ya kuwashambulia kwa matusi na kipigo dereva wa gari na abiria wake.

Tukio hilo lilianza kusambazwa juzi kwenye mitandao ya kijamii kupitia video fupi inayowaonyesha watu wawili wenye sare za Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani, wakiwatukana matusi na kuwapiga dereva na abiria wake wakati walipokuwa wakishuka kwenye gari.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni, alitoa agizo la kukamatwa kwa askari hao juzi, akieleza kuwa wamekosa uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao.

 

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, wakati wa uzinduzi wa mafunzo na uchoraji picha za usalama barabarani yanayotolewa na Kampuni ya Mafuta ya Puma kwa wanafunzi wa shule za msingi nchini, Masauni alisema kitendo kilichofanywa na askari wake hakikubaliki ndiyo maana wamewachukulia hatua dhidi yao.

Masauni alisema kumekuwa na malalamiko mengi ya madereva kubambikwa makosa au askari kufanya vitendo vilivyo kinyume cha mwenendo mwema wa jeshi hilo, na walipoona tukio hilo, watachukulia hatua dhidi ya askari hao mara moja.

Naibu waziri huyo alisema askari polisi wanaotuhumiwa kufanya tukio hilo wanashikiliwa na jeshi hilo, wakati wakisubiri taratibu za kisheria.Alisema vitendo vinavyolalamikiwa na wananchi dhidi ya Jeshi la Polisi ni pamoja na askari wake kupokea rushwa, lugha chafu kwa madereva na kuwashambulia.

“Jana (juzi) kuna video ambayo ilikuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikiwaonyesha askari wakimtukana dereva pamoja na abiria waliokuwamo," Masauni alisema.

 

"Na si hivyo tu, ilifika hatua hadi kumpiga. Baada ya tukio hili, nilimwagiza Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani achukue hatua kwa suala hili.

"Jana (juzi) nilipewa taarifa wamekamatwa askari waliofanya kitendo kile na wamewekwa ndani na sasa wanasubiri kufikishwa kwenye vyombo vya sheria."

Alisema watuhumiwa wanashikiliwa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, huku akiwataka wananchi kutoa taarifa pindi wanapoona kuna vitendo viovu vinafanywa na askari polisi.

Alisisitiza kuwa ikitokea uongozi wa jeshi hilo unatetea au kutochukua hatua stahiki, mlalamikaji awataarifu viongozi wa juu wa wizara.

“Ninawaasa askari wote kuwa serikali iko makini na haitaruhusu mwananchi yeyote aonewe na vyombo vya dola. Pia hatutaruhusu mwananchi au taasisi yoyote imuonee askari kwa sababu yoyote ile," Masauni alisema.

Masauni pia aliipongeza Kampuni ya Mafuta ya Puma kwa kuendesha programu hiyo na kuzitaka kampuni nyingine kuiga mfano huo kwa kuwekeza kwenye ulinzi na usalama wa watoto ambao ni taifa la leo na kesho.

Habari Kubwa