Askari sasa kusindikiza mabasi ya abiria

19Jan 2022
Paul Mabeja
KONGWA
Nipashe
Askari sasa kusindikiza mabasi ya abiria

JESHI la Polisi mkoani Dodoma, linaanza utaratibu wa kutumia askari wake kusindikiza mabasi ya abiria ili kukabiliana na ajali zinazotokana na mwendo kasi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Onesmo Lyanga, alibainisha hayo juzi wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ajali ya basi la abiria la kampuni ya Baraka Classic lenye namba za usajili T967 DWW, iliyotokea eneo la Pandambili, wilayani Kongwa, mkoani Dodoma.

Katika ajali hiyo watu watatu walifariki dunia na wengine 11 kujeruhiwa.

Kamanda Lyanga, alisema ili kukabiliana na ajali zitokanazo na mwendokasi wa madereva wa mabasi ya abiria Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, linapanga kuanza kutumia askari kusindikiza mabasi ya abiria yaendayo mikoani.

“Kuanzia sasa katika mkoa wetu wa Dodoma tutaanza kutumia askari kusindikiza basi ambalo litakuwa la kwanza kuondoka stendi asubuhi na ni marufuku kwa mabasi yatakayotoka nyuma kulipita basi hilo hii itasaidia kudhibiti masuala ya mwendo kasi kwa madereva wa mabasi,” alisema Kamanda Lyanga.

Akizungumzia tukio la ajali hiyo katika eneo la tukio Kamanda Lyanga, alisema basi hilo ambalo lilikuwa likitoka Dodoma kwenda Dar es Saalam, chanzo ni mwendo kasi licha ya kuwapo hali ya hewa ya mvua.

Alisema kuwa basi hilo lilipata ajali kutokana na mwendo kasi hali ambayo ilisababisha kupoteza mwelekeo na kwenda kukita katika kingo ya barabara.

“Hali ya barabara haikuwa mbaya sana, lakini chanzo ambacho kimesababisha ajali hii ni mwendo kasi wa dereva wa basi hili na watu 11 wamejeruhiwa na wengine watatu wamepoteza maisha,” alisema.

Kadhalika, alisema kati ya watu hao watatu waliofariki, wawili wameshatambuliwa na miili yao imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro.

“Kati ya hawa watatu waliofariki mmoja ametambulika kwa jina la Salha Mohamed, mwanafunzi wa kidato cha pili, mkazi wa Dar es Saalam na Joyce Nyaula, mtu mzima naye mkazi wa Dar es Saalam, huyo mmoja bado hajatambuliwa,” alisema Kamanda Lyanga.

Vilevile, alisema majeruhi 10 wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya Kongwa kwa ajili ya matibabu na mmoja wao amekimbizwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa matibabu zaidi.

Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Remidius Emmanuel, aliwataka wananchi wanaotumia usafiri wa mabasi kutoa taarifa za madereva wanaoendesha vyombo vya moto kwa mwendo kasi.

“Kwa madereva sasa ni msimu wa mvua, hivyo wawe makini, lakini viongozi wa maeneo ambayo yapo jirani na barabara kuu kuhakikisha kuwa wanatoa taarifa za ajali pindi zinapotokea,” alisema Emmanuel.

Habari Kubwa