Askofu alaani wanaosaini mikataba kifisadi

27Jun 2017
George Tarimo
IRINGA
Nipashe
Askofu alaani wanaosaini mikataba kifisadi

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT ), Fredrick Shoo, amewalaani  viongozi wa serikali wanaopewa maradaka na kuyatumia vibaya kwa kukaa na mabepari nje ya nchi na kusaini mikataba ya ovyo ambayo inawaumiza Watanzania na kuwaibia. 

MKUU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT ), Fredrick Shoo akiwa na Rais john Magufuli katika moja ya ibada za jumapili.picha na maktaba

Shoo ameyasema hayo juzi wakati wa kumsimika Askofu mpya wa Dayosisi ya Iringa, Braston Gaville.

Askofu Shoo alisema kuna watu wanatumia madaraka vibaya, wanasaini mikataba ya ovyo, lakini amempongeza Rais John Magufuli kwa kuwashughulikia watu hao ambao wanajifanya nimiungu watu.

“Heshima ya kiongozi yeyote wa serikali na viongozi wa dini ni pale wanapowatumikia wananchi bila kujali dini, vyeo wala kabila na hivyo ndivyo uongozi unavyotakiwa kwa viongozi kuwatumikia wananchi,” alisema askofu Shoo. 

Naye askofu mpya Gaville alisema wananchi na waumini wanatambua mchango mkubwa wa serikali ya awamu ya tano ya Rais Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya.

Gaville alisema serikali ya awamu ya tano inafanya kazi ya kuwatetea wanyonge na Taifa na kuwa wanyonge ni wengi kuliko wasio wanyonge.

Alisema dayosisi itaendelea kushirikiana na serikali pamoja na wadau wengine wa maendeleo kuleta maendeleo katika taifa. 

Katika hatua nyingine, alisema anaamini uongozi wa awamu ya tano ambao ni makini, utaendelea na mchakato wa kuandika katiba mpya ambao ulishauanza. 

Pia Gaville alisema umoja na ushirikiano ndio utakaoliletea taifa maendeleo huku akiahidi kuwa dayosisi yake kushirikiana na vyama vyote vya siasa.

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamhuri David, alimpongeza askofu mstaafu Owndeburg Mdegella, kwa kukubali kubadilishana uongozi na askofu mpya kwa sababu makanisa mengi yanaingia kwenye migogoro wanapotaka kubadilisha uongozi. 

Habari Kubwa