Askofu atoa hadhari corona

30May 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Askofu atoa hadhari corona

ASKOFU wa Kanisa la Waadvetista Wasabato Jimbo la Kusini, Mark Malekana, amewataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya virusi ya corona licha ya Tanzania kufanikiwa kupunguza maambukizo.

Amesema Rais John Magufuli amesaidia kuondoa na kumaliza hofu iliyokuwa imetanda nchini ambayo ilikuwa ikiondoa maisha ya Watanzania na kufanya maambukizo kupungua.

Askofu Malekana alitoa wito huo jana jijini Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari katika hafla ya kukabidhi vifaa vya kujikinga na maambukizo ya virusi vya corona zikiwamo barakoa, vitakasa mikono na vifaa vya kujikinga vya wataalamu wa afya vyenye thamani ya Sh. milioni nane kwa Manispaa ya Temeke.

Alisema misaada hiyo ni mwendelezo wa misaada yenye thamani ya Sh. milioni 100 iliyotolewa na Shirika la Maendeleo na Misaada Wakati wa Maafa la Kisabato (Adra Tanzania) kwa udhamini wa Taasisi ya LDS.

Alisema jitihada hizo zinakwenda sambamba na kuchapisha vipeperushi vya kutoa elimu kwa jamii kujikinga na maambukizo hayo.

"Ujasiri usiwaondolee tahadhari, tumetiwa moyo ili tusife kwa hofu ya corona. Tuendelee kuzingatia tahadhari zinazotolewa na Wizara ya Afya na tuache kupokea taarifa kutoka vijiweni, masokoni na watu wasiohusika katika hili," Askofu Malekana alionya.

Kiongozi huyo wa kiroho pia aliwataka Watanzania kuendelea na utaratibu wa kunawa mikono mara kwa mara kwa sababu unaepusha maradhi mbalimbali ya kuambukiza.

Vilevile, alivitaka vyuo vyote na wamiliki wa shule za sekondari na msingi nchini, kutoingilia ratiba za kumwabudu Mungu katika siku zilizopangwa kwa waumini wa dini zote kwa kisingizio cha ratiba za masomo kubana.

"Vyuo na shule zinaanza kufunguliwa tunawaomba wahusika wote kuzingatia ratiba za kumuabudu Mungu na siyo walimu wanaanza kupanga ratiba za masomo na mitihani na kutoweka siku za kuabudu kwa kisingizio muda hautoshi, tuheshimu ratiba za kumwabudu Mungu maana bila yeye tusingeishinda hofu iliyokuwa mbele yetu," alisema.

Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Manispaa ya Temeke, Grace Ntangu, aliwashukuru kwa msaada waliowapatia na kuahidi kuwafikia walengwa wote.

Habari Kubwa