Askofu Isuja alishona mavazi ya kuzikwa nayo

21Apr 2016
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Askofu Isuja alishona mavazi ya kuzikwa nayo

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Dodoma, Beatus Kinyaiya, amesema Askofu mstaafu wa Kanisa Kuu la katoliki Jimbo la Katoliki Dodoma, alishona mavazi kwa ajili ya mazishi yake.

Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa akitoa heshima za mwisho jana katika mazishi ya aliyekuwa Askofu wa kwanza mzalendo kanisa Katoliki jimbo la Dodoma Mathias Isuja.

Askofu Mkuu Kinyaiya aliyasema hayo jana, wakati wa mahubiri ya ibada ya maziko ya Askofu Isuja, yaliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulio wa Msalaba, mjini hapa.

Alisema wakati wa uhai wake, Isuja alifanya maandalizi yake kwa kujishonea nguo za kuzivaa wakati wa kuzikwa, atakapokufa.

“Marehemu Isuja alikuwa haogopi kifo ndiyo maana alikuwa na ujasili wa kujishonea nguo kwa ajili ya maandalizi ya kumvisha baada ya kufa kwake. Pia aliagiza azikwe ndani ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, Askofu Mkuu Kinyaiya aliwataka waumini wote wa kanisa hilo kumuiga kimatendo Askofu Isuja kwa kutenda mema kila wakati.

Isuja ambaye alikuwa askofu wa kwanza Mtanzania katika Jimbo la Dodoma (sasa jimbo kuu), alifariki dunia Aprili 13, mwaka huu, katika hospitali ya Misheni ya Itigi, Singida, na kuzikwa ndani ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba, la Jimbo Kuu la Dodoma.

Katika maziko hayo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwaongoza mamia ya waumini wa Kanisa hilo na madhehebu mengine.

Akizungumza kwa niaba ya Rais Dk. John Magufuli, Majaliwa alisema serikali imepokea kifo hicho kwa masikitiko kutokana na juhudi za maendeleo alizokuwa akizifanya Askofu Isuja wakati wa uhai wake.

Naye Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, alisema Askofu Isuja ni kati ya viongozi ambao walifanya kazi katika mkoa wa Dodoma katika mazingira magumu lakini hakukata tamaa.

Habari Kubwa