Askofu mbaroni tuhuma za mauaji

22Apr 2018
Allan lsack
ARUSHA
Nipashe Jumapili
Askofu mbaroni tuhuma za mauaji

ASKOFU wa Kanisa la International Evangelism, Eliud Isangya (69), anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kwa tuhuma za mauaji ya aliyekuwa Mchungaji wa Kanisa la African Mission, Nixon Ndeleko (71).

ASKOFU wa Kanisa la International Evangelism, Eliud Isangya.

Akizungumza na Nipashe juzi, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Yusuf Ilembo, alisema jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa watatu waliohusishwa na tukio hilo la mauji.

Mbali na Isangya, Kamanda Ilembo aliwataja watuhumiwa wengine kuwa ni Ndelekwa Isangya (59) ambaye ni ofisa mwandamizi wa kanisa hilo na Obadia Nanyaro (60) mlinzi wa kanisa.

Aidha, Ilembo alisema tukio la mauji lilitokea Januari Mosi, mwaka 2017, katika eneo la Moivaro, jijini Arusha.

Alisema mwili wa marehemu ulikutwa nyumbani kwake ukiwa na majeraha yaliyosababishwa na kuchomwa na kitu chenye ncha kali huku akiwa ameshindiliwa nguo mdomoni.

Kamanda huyo alisema jeshi la polisi liliendelea na upelelezi wake na kwamba Aprili 17, mwaka huu, mtuhumiwa mmoja (jina limehifadhiwa) alikamatwa na baada ya kuhojiwa na polisi alitoa ushirikiano na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wengine.

Licha ya kuwashikilia watuhumiwa hao, alisema Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi wa tukio hilo. 

Habari Kubwa