Askofu Mdegella ataja sifa za uongozi wa kuchaguliwa

14Jul 2020
Francis Godwin
Iringa
Nipashe
Askofu Mdegella ataja sifa za uongozi wa kuchaguliwa

ASKOFU mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Dk. Owdenburg Mdegella, amesema jamii inahitaji kuwa na viongozi wabeba maoni yao na si wanaotafuta kuitumia jamii kupata mali.

Akizungumza jana wakati wa kipindi chake kinachorushwa na Radio Furaha na kituo cha matukio Daima Tv, Dk. Mdegella alisema kuwa suala la uongozi linahitaji mtu mwenye utayari wa kweli wenye uchaji wa kimungu katika kuwatumikia wananchi.

Dk. Mdegella ambaye ni mtiania wa ubunge Jimbo la Kilolo mkoani Iringa, alisema kuwa kwa upande wake haingii kuomba nafasi ya ubunge ili kwenda kujinufaisha bali anakwenda kuitumikia jamii.

Alisema kuwa upande wake amejitosheleza kwa mali mbalimbali anazomiliki yakiwamo mashamba, nyumba na magari na kuwa haendi katika ubunge kwa ajili ya kutafuta mali bali anakwenda kiwito kwenda kuwatumikia wananchi ili nao wafurahie matunda ya nchi yao na jitihada za serikali ya CCM chini ya Rais John Magufuli.

Alisema katika hali ya kawaida, uongozi wa kisiasa mtu yeyote anaweza kubahatisha, lakini sio uongozi wa kumtumikia Mungu ingawa asema wote wasaka uongozi ni vema wakajiuliza mbele za Mungu juu ya nafasi wanazoomba iwapo wanaweza kuzitumikia.

Dk. Mdegella alisema kila mmoja anamapungufu yake ya kibinadamu, lakini hakuna sababu ya kukata tamaa kutokana na mapungufu hayo badala yake kusonga mbele na kumtanguliza Mungu kwa kila hatua.

Habari Kubwa