Askofu Mkude amewataka wazazi kuwalea watoto wao kimaadili

20Sep 2020
Christina Haule
Morogoro
Nipashe
Askofu Mkude amewataka wazazi kuwalea watoto wao kimaadili

MHASHAMU Askofu wa Jimbo katoliki Morogoro, Askofu Telesphory Mkude, amewataka wazazi hasa wa Kike kuendelea kuwalea watoto kimaadili ili wamjue Mungu na kujiepusha na mambo yasiyofaa.

Mhasham Askofu Telesphory Mkude akibariki kwa ajili ya uzinduzi ofisi ya Redio Maria iliyopo kwenye parokia ya Mtakatifu Maria Jimbo Katoliki Morogoro.

Askofu Mkude amesema hayo jana wakati wa uzinduzi wa Ofisi ya Redio Maria kanda ya Morogoro zilizopo kwenye kanisa Katoliki la Mtakatifu Maria Modeko Mkoani hapa ambapo amesema siku zote mama anapaswa kutambua kuwa ndiye Katekista wa kwanza wa mafundisho ya mambo ya Mungu kwa mtoto kabla ya Katekista wa Kanisani.

Amesema wazazi wananafasi kubwa ya kuwalea watoto katika maadili mema na ya kumpendeza Mungu na hivyo kuwa katika njia zinazompendeza Mungu.

“Sisi Sote ni Watoto wa Mungu na kwa sababu Yesu ni mwana wa Mungu, sisi sote ni wana wa Mungu na hivyo ni wana wa Mama Bikira Maria, hivyo wazazi hawana budi kuwalea Watoto kama mama Maria alivyomlea vyema mtoto Yesu” amesema Askofu Mkude.

Hata hivyo amewataka wazazi kuwazoesha watoto wao kusikiliza Redio za dini ikiwemo Redio Maria, Redio Ukweli na Redio Vatican ili wajifunze mambo muhimu ya kumjua Mungu na kuyaishi.

Amesema Redio za kanisa zina nafasi kubwa ya kuielimisha Jamii ikiwemo Watoto hata wawapo majumbani juu ya mambo ya kumpendeza Mungu.

Naye Katibu wa Halmashauri ya walei Parokia ya Modeko, Martha Mkoma, ameupongeza uongozi wa Redio Maria makao makuu kwa kufungua Ofisi katika Parokia ya Mtakatifu Maria - Modeko ambapo hiyo ni heshima kubwa kwao wanaparokia ya Modeko kwa kuukaribisha Utume wa Redio Maria.

Habari Kubwa