Askofu Mokiwa ashangaa viongozi wa dini kutohoji maamuzi ya Jecha

16Mar 2016
Rahma Suleiman
Nipashe
Askofu Mokiwa ashangaa viongozi wa dini kutohoji maamuzi ya Jecha

ASKOFU wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk. Valentino Mokiwa, ameshangazwa na kitendo cha viongozi wa dini kukaa kimya dhidi ya hatua ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) uchaguzi wa Zanzibar.

Askofu Dk. Valentino Mokiwa.

Alisema viongozi wa dini wanatakiwa kusema ukweli na walitakiwa kuhoji ni kwanini Zec ilifuta matokeo yote ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, lakini jambo hilo halikufanyika, badala yake viongozi wa dini walikaa kimya.

Alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa viongozi wa madhehebu kadhaa ya dini na kuwataka viongozi wa dini kutogawanyika kwa itikadi za kisiasa na kujitahidi kuhubiri amani na utulivu wa nchi kwani amani ikitoweka ni vigumu kuirejesha.

Askof Mokiwa ambaye pia ni Rais wa Mabaraza ya Makanisa ya Afrika, alisema linapotokozea tatizo katika nchi, ni lazima viongozi wa dini kuwa kitu mikoja na kutafute njia za kutatua matatizo hayo.

Aidha, alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kutotumia nguvu zaidi kwa kuwa Zanzibar ipo katika hali ya amani na utulivu.

Alisema kwa kutumia nguvu zaidi za vyombo vya dola kunaweza kunawajengea hofu wananchi hasa wanapoona vifaru vya kijeshi vinapotembea barabarani wakati hali ni shwari.

Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar, Khamis Yussuf, alilitaka Jeshi la Polisi kukidhibiti kikundi kinachopiga raia ambao hawana hatia kijulikanacho kwa jina la Mazombi.

Alisema kuendelea kuwapo kwa kikundi hicho kutajenga chuki na uhasama, hivyo kusababisha vunjifu wa amani kutokana na wanaopigwa au familia zao zitataka kulipiza visasi.

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum, alisema watu wote wapewe heshima yao na wasibugudhiwe kutokana na kushiriki au kutoshiriki kwao katika uchaguzi wa marudui wa Zanzibar Jumapili ijayo.

Alisema Zec ndiyo iliyotangaza uchaguzi wa marudio, hivyo tume hiyo inatakiwa iwe na uadilifu, isimamie haki, sheria, kanuni na taratibu ili uchaguzi uwe wa haki na huru.

“Haitakuwa jambo la busara kama Wazanzibari wataanzisha fitina za nyuma za siasa za chuki na uhasama kulikosababisha kushindwa kusaidiana kutokana na itikadi za kisiasa,”alisema Shekhe Salum bila kueleza uchaguzi huo utakuwaje huru na haki wakati utakihusisha CCM na vyama ambavyo havina wafuasi kutokana na CUF kutoshiriki.

Habari Kubwa