Askofu Mwamakula, Lwaitama mbaroni

18Jul 2021
Romana Mallya
Mwanza
Nipashe Jumapili
Askofu Mwamakula, Lwaitama mbaroni

​​​​​​​JESHI la Polisi mkoani Mwanza linawashikilia watu 38, wakiwamo viongozi wa Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kiongozi wa dini kwa tuhuma za kufanya mkutano wa kudai Katiba Mpya bila kibali.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ramadhani Ng'anzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ramadhani Ng'anzi, aliiambia Nipashe jana kuwa miongoni mwa wanaowashikilia, wamo wanawake sita.

Aliwataja wanaowashikiliwa kuwa ni pamoja na Askofu Emmaus Mwamakula wa Kanisa la Uamsho Moravian, ambaye Kamanda huyo alidai aliliambia Jeshi la Polisi kuwa alikwenda kwa ajili ya kuombea mkutano huo.

“Ni kweli tunawashikilia baadhi ya wafuasi na miongoni mwao wapo viongozi wa BAVICHA kwa kufanya mkutano wa hadhara bila kutoa taarifa kituo cha polisi na kuruhusiwa," alisema.

Aliwataja wengine wanaowashikilia kuwa ni Katibu Mwenezi wa Vijana Taifa, Mhadhiri mstaafu, Dk. Azaveli Lwaitama.

“Hawa ninawakumbuka vizuri kwa majina yao. Kwa sasa nipo nje ya ofisi, majina ya wengine siyakumbuki,” Kamanda huyo alisema katika mazungumzo na Nipashe kwa simu.

Kamanda Ng’anzi alidai kuwa juzi watuhumiwa hao walifanya matangazo mtaani kuujulisha umma kuwa jana kungelifanyika kongamano la kudai Katiba Mpya na kuwataka wananchi wahudhurie kwenye ukumbi waliopanga kufanya mkutano huo.

“Kwa kuwa walikuwa wameshaondoka katika uanachama na kila mtu anaruhusiwa kuhudhuria, tukazuia wasifanye kongamano hilo hadi watakapopata kibali cha polisi kwa sababu wametoka kwenye uanachama wamekwenda kwa kila mtu.

“Tuliwaandikia barua jana (juzi) jioni wasifanye mkutano baada ya gari la matangazo kupita mtaani, tuliwajulisha kwamba mkutano wa ndani hauna matangazo na walikuwa hawasemi wanachama bali wananchi wote waende kwenye kongamano,” alisema.

Kamanda huyo alisema wananchi wengi walitii amri ya polisi na hawakuhudhuria, lakini wachache walikaidi, hivyo wanashikiliwa.

“Tunawahoji kujua ni kwa nini wanakusanyika baada ya kuwaambia wasikusanyike. Endapo ushahidi utatosheleza, tuna uwezekano wa kuwafikisha mahakamani kwa kufanya kusanyiko lisilokuwa halali," alisema.

Alisema endapo hawatatimiza masharti ya dhamana, ushahidi ukikamilika au kujitosheleza watashtakiwa.

Habari Kubwa